Sep 11, 2018 11:45 UTC
  • Kamanda wa Jeshi la Iran: Iraq iwakabidhi magaidi wanaoshambulia ardhi ya Iran

Kamanda wa Majeshi ya Iran amesema kuwa Marekani imekuwa ikiyachochea makundi ya kigaidi yaliyoko eneo linalojiendeshea mambo yake la Kurdistan nchini Iraq ili yashambulie ardhi ya Iran licha ya kwamba yameahidi kutofanya hivyo.

Meja Jenerali Mohammad Baqeri ameashiria mashambulizi ya makombora yaliyofanywa na Iran Jumamosi iliyopita dhidi ya ngome ya kundi moja la kigaidi katika eneo la Kurdistan nchini Iraq na kusema kuwa, taifa la Iran lina haki ya kujilinda. 

Amesema tangu mwaka 1996 viongozi wa eneo la Kurdistan huko Iraq na wale wa Chama cha Kurdistan Democratic waliahidi kimaandishi kwamba hawatashambulia ardhi ya Iran, lakini wametupilia mbali na kukiuka ahadi yao kutokana na uchochezi wa Marekani na kufanya mashambulizi ya kigaidi.

Meja Jenerali Baqeri amesema jambo hilo halikubaliki na kwamba iwapo mashambulizi kama hayo yatakariri yatakabiliwa na jibu kali zaidi kutoka Iran. 

Amesema kuwa serikali ya Iraq na utawala wa eneo la Kurdistan hawapaswi kuruhusu mashambulizi kama hayo ya kigaidi dhidi ya Iran na kwamba wanapaswa kuwakabidhi magaidi hao kwa serikali ya Tehran au kwa uchache kuwafukuza katika ardhi ya Iraq.

Makombora saba yamelenga ngome za kundi la kigaidi nchini Iraq.

Itakumbukwa kuwa, Jumamosi iliyopita Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilijibu hujuma za magaidi hao kwa kushambulia kwa makombora saba ya masafa mafupi makao na mkutano wa viongozi wa kundi moja la kigaidi na vilevile kituo chao cha mafunzo katika eneo la Kurdistan nchini Iraq. 

Maoni