Sep 18, 2018 11:36 UTC
  • Sisitizo la IAEA la kutekeza Iran makubaliano ya nyuklia; na njama mpya za Donald Trump dhidi ya JCPOA

Makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) yalitiwa saini Julai 2015 mjini Vienna Austria baina ya Iran na kundi la 5+1, linaloundwa na Marekani, Uingereza, Ufaransa, China, Russia pamoja na Ujerumani na kuanza kutekelezwa Januari 2016.

Asasi ya kimataifa inayosimamia utekelezaji ahadi wa Iran kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ambao umetangaza kuwa, Iran imetekeleza ahadi zake na kufungamana kikamilifu na makubaliano hayo ya kimataifa. Yukiya Amano, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) amesisitiza kuwa, makubaliano hayo yamekuwa na mafanikio makubwa.

Akihutubia katika siku ya kwanza ya kikao cha 62 cha Baraza Kuu la Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) Amano alibainisha kwamba, tangu kufanyikka kikao cha mwisho cha baraza hilo, wakala huo imesimamia na kuchunguza ahadi za Iran kuhusiana na makubaliano ya nyuklia na kusisitiza kwamba: Iran imefungamana kikamilifu na suala la utekelezaji wa ahadi zake kuhusu makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) na ni muhimu kwa Tehran kuendelea kufungamana na utekelezaji wa ahadi zake katika uwanja huo.

Wakala wa kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA)

Licha ya ripoti zote za Wakala wa kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kusisitiza kwamba, Iran imetekeleza majukumu yake na kufungamana kikamilifu na makubaliano ya JCPOA, lakini Rais Donald Trump wa Marekani iwe ni katika kipindi cha kampeni za kugombea urais au hata baada ya kuingia katika ikulu ya White House daima amekuwa akiyakosoa vikali makubaliano hayo na kuyataja kuwa makubaliano mabaya kabisa. Hatimaye tarehe 8 Mei mwaka huu, Trump alichukua uamuzi wa kuiondoa nchi yake katika makubaliano hayo na kisha kuiwekea vikwazo vipya vya nyuklia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kwa hakika Wamarekani wanafahamu bayana kwamba, Iran imetekeleza ahadi na majukumu yake yote katika fremu ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, lakini pamoja na kuelewa wazi hilo wakiwa na lengo la kuhalalisha hatua zao, wamekuwa wakieneza tuhuma na urongo dhidi ya Iran. Hatua ya hivi karibuni kabisa katika uwanja huo, ni ujumbe wa Donald Trump kwa ajili ya mkutano wa 62 wa Baraza Kuu la IAEA uliosomwa na Rick Perry, Waziri wa Nishati wa Marekani ambapo ulitoa masharti mawili kwa Iran.

Rais Donald Trump wa Marekani ambaye ni mpinzani mkuu wa makuubaliano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA

Katika ujumbe huo Trump amesema: Iran inapaswa kutoa dhamana ya  masuala mawili. Mosi, miradi yake ya nyuklia itabakia kuwa ni ya amani na pili ni kuwa, njia yoyote ile ya Iran ya kuelekea katika kutengeneza silaha za nyuklia itafungwa milele. Trump hakuashiria katika ujumbe wake huo kuhusu kujitoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia lakini akasisitiza kwamba, JCPOA ni "makubaliano yenye mapungufu".  Aidha amesema kuwa, Marekani inafuatilia suala la kufikia makubaliano kamili kuhusiana na miradi ya nyuklia ya Iran  na vile vile harakati eti za Tehran za kuhatarisha amani na uthabiti.

Akibainisha sababu za kuwa na mapungufu makubaliano ya sasa ya nyuklia ya JCPOA, Waziri wa Nishati wa Marekani amesema kuwa, makubaliano ya JCPOA hayajajishughuulisha kabisa na utendaji mbaya unaoendelea wa Iran, hata kama utendaji mbaya huo kidhati si wa nyuklia.

Kwa hakika lengo hasa la Trump la kutoa ujumbe huo na kuonyesha utakaji makuu wake ulio nje ya ahadi za Iran katika fremu ya makubaliano ya nyuklia  ya JCPOA, ni kubinya shughuli za miradi ya nyuklia ya Iran zenye malengo ya amani na hatimaye kusitisha kikamilifu miradi hiyo kwa maslahi na matakwa ya utawala haramu wa Israel. 

Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran

Hii ni katika hali ambayo, jamii ya kimataifa hususan wanachama wote waliobakia katika kundi la 5+1 wanataka kulindwa na kubakishwa makubaliano hayo. Katika fremu hiyo, Umoja wa Ulaya umetoa kifurushi cha mapendekezo kwa minajili ya kuishajiisha Iran ibakie katikka makubaliano hayo.

Kinyume na azma ya jamii ya kimataifa na ikichukua hatua ya upande mmoja, Marekani inataka kutwisha mitazamo na matakwa yake kupitia njia ya mashinikizo na kuiwekea vikwazo Iran.

Pamoja na hayo, hivi sasa hata washirika wa Ulaya wa Marekkani wamekiri bayana kwamba, hatua ya Trump ya kuiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ilikwenda kinyume kabisa na ahadi za Washington katika kipindi cha utawala wa Rais Barack Obama ilizozitoa kwa mujibu wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kadhalika hatua hiyo ya Trump inakinzana na msingi mkuu wa sheria za kimataifa yaani ulazima wa kutekeleza ahadi zilizotolewa na serikali mbalimbali.

Tags

Maoni