Sep 19, 2018 04:43 UTC
  • Mamilioni washiriki kumbukumbu ya Tasuaa Iran na maeneo mengine ya dunia

Mamilioni ya Waislamu wa Iran na maeneo mengine ya dunia usiku wa kuamkia leo tarehe 9 Mfunguo Nne Muharram wameshiriki katika vikao, majlisi na shughuli za maombolezo na kukumbuka misiba na masaibu yaliyomkuta mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali (as), ndugu na mswahaba zake waaminifu huko Karbala nchini Iraq mwaka 61 Hijria.

Katika shughuli hiyo ya tasua'a, mamilioni ya Wairani wapenzi na maashiki wa Imam Hussein na watu wa familia ya Mtume Muhammad (saw) waliokuwa wamevaa nguo nyeusi kama ishara ya huzuni na maombolezo wamemkumbuka Abul Fadhl Abbas bin Ali, ndugu yake Imam Hussein ambaye ndiye aliyekuwa mbeba bendera na kamanda wa jeshi la mtukufu huyo katika mapambano ya siku ya Ashuraa.

Mjini Tehran majlisi za maombolezo na kuwakumbuka mashujaa wa Karbala hususan Abul Fadhl zimefanyika katika maeneo mbalimbali ikiwemo ile iliyofanyika katika Husseiniya ya Imam Khomeini na kuhudhuriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei. 

Ayatullah Khamenei katika majlisi ya Tasuaa, Tehran.

Katika siku ya 9 ya mwezi Muharram mahatibu na wazungumzaji humkumbuka zaidi Abbas, Abul Fadh ambaye alionesha ushujaa, wa hali ya juu katika mapambano ya Karbala na kuwakumbusha watu ushujaa usio na kifani wa baba yake, Ali bin Abi Twalib (as). Abul Fadhl al Abbas aliuawa shahidi siku ya tarehe kumi Muharram baada ya kukatwa mikono miwili na maadui wa Watu wa Nyumba ya Mtume wetu Muhammad (saw) wakiongozi na Yazid bin Muawiya.

Watu 72 waliokuwa Karbala wote waliuawa shahidi wakiwa pamoja na kiongozi wao, Imam Hussein bin Ali (as) katika mapambano ya haki dhidi ya dhulma na uonevu.   

Maoni