• Maafikiano ya Sochi na uungaji mkono wa Iran kwa utumizi wa diplomasia kutatua kadhia ya Idlib

Makubaliano yaliyofikiwa mjini Sochi kati ya Russia na Uturuki kuhusu kadhia ya eneo la Idlib lililoko kaskazini magharibi mwa Syria baada ya kikao kilichofanyika mjini Tehran kati ya marais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia na Uturuki yamekaribishwa na kuungwa mkono na Iran. Maafikiano hayo ni ishara ya mwendelezo wa njia athirifu za kidiplomasia.

Kutokomezwa kikamilifu magaidi katika ardhi ya Syria ndilo lengo kuu la serikali ya nchi hiyo, ambapo kati ya njia mbalimbali zilizotumika hadi sasa mbinu ya diplomasia imekuwa na taathira kubwa zaidi. 

Kutokana na muundo tata uliopo wa idadi ya watu katika mkoa wa Idlib huku magaidi na makundi ya upinzani yanayobeba silaha yakiwa yamechanganyika na raia wa kawaida, kulinda maisha ya raia hao ndilo suala linalopewa umuhimu wa kwanza katika operesheni za kuitokomeza ngome ya mwisho ya magaidi katika ardhi ya Syria. Hiyo ni nukta ambayo marais wa Iran, Russia na Uturuki waliijadili na kuitilia mkazo katika kikao walichofanya karibu wiki mbili nyuma hapa mjini Tehran, ambapo makubaliano rasmi juu ya suala hilo yamefikiwa kwenye "Maafikiano ya Sochi" kwa mashauriano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kutoka kushoto: Rais Hassan Rouhani wa Iran, Rais Vladimir Putin wa Russia na Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki katika kikao cha Tehran

Mnamo siku ya Jumatatu, marais Vladimir Putin wa Russia na Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki walifikia makubaliano mjini Sochi, Russia ya kughairisha operesheni ya kijeshi katika mkoa wa Idlib ili kulinda maisha ya raia na wakati huohuo kutenga eneo lisilo la kijeshi ndani ya mkoa huo ili kuweza kuwatimua na kuwatokomeza kikamilifu magaidi katika eneo hilo la mwisho la ardhi ya Syria pasi na kusababisha madhara kwa raia. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Iran imeyaunga mkono Maafikiano ya Sochi licha ya kutotuma mwakilishi kwenye kikao hicho, huku ikisisitiza kwamba huo ni mwendelezo wa mchakato wa mazungumzo ya Astana na kikao cha Tehran. Kuwepo hakikisho la kuhitimishwa harakati za misimamo ya kufurutu mpaka na uwepo wa magaidi katika mkoa wa Idlib, ni takwa linalotiliwa mkazo na serikali halali ya Syria ili kuweza kulinda umoja wa ardhi yote ya nchi hiyo; na kufikiwa lengo hilo muhimu sambamba na kuepusha madhara makubwa kwa raia wa kawaida ndilo takwa la nchi tatu za Iran, Russia na Uturuki zinazosimamia "Mchakato wa Astana". Kwa hivyo kuendeleza mwenendo huo ni kielelezo cha taathira chanya za udiplomasia. Akizungumzia maafikiano ya Sochi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema huo ni mwendelezo wa mashauariano yaliyofanyika Ankara, Damascus na kwenye kikao cha Tehran na akaongezea kwa kusema: "Diplomasia hii amilifu itapelekea kuzuia kutokea vita Idlib".

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif

Bahram Qassemi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, naye pia amekaribisha maafikiano ya Russia na Uturuki katika kikao cha Sochi na kueleza kwamba: "Kikao cha viongozi wa Russia na Uturuki na kutangazwa makubaliano kuhusu jinsi ya kutatua kadhia ya Idlib, ni hatua ya msingi katika harakati ya kutokomeza mabaki ya magaidi nchini Syria." Gholamali Khoshroo, mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa, yeye amesema kuhusiana na maafikiano ya Sochi kwamba: "Maafikiano haya yanatokana na njia ya msingi na moyo uliotawala kwenye mchakato wa Astana, ambapo mbali na kuendeleza mapambano dhidi ya magaidi, inapasa zifanyike jitihada zinazohitajika kuepusha maafa kwa raia.

Mabaki ya magaidi katika ardhi ya Syria

Misimamo yote hii inaonyesha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaheshimu msingi muhimu wa kulinda maisha ya raia wakati wa kulisafisha eneo la Idlib kwa kuyatokomeza magaidi yaliyopiga kambi kwenye mkoa huo wa ardhi ya Syria; na ndiyo maana imeunga mkono maafikiano ya Sochi ambayo hatimaye yatahitimisha uwepo wa magaidi huko Idlib. Ushirikiano wa Iran, Russia na Uturuki kupitia mchakato wa mazungumzo ya Astana umewezesha mapambano dhidi ya magaidi nchini Syria kufikia kwenye ngome ya mwisho ya magaidi hao huko Idlib. Na ndiyo kusema kuwa hatua yoyote ile itakayopendekezwa kuchukuliwa kwa mashauriano ya nchi hizo tatu kwa ajili ya kutatua suala hilo la makao ya mwisho ya magaidi nchini humo itakuwa na hakikisho la utekelezaji. Kuhusiana na suala hilo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif na mwenzake wa Uturuki Mevlut Cavusoglu jana Jumanne walifanya mazungumzo kwa njia ya simu na ikaafikiwa kwamba maelezo zaidi kuhusiana na "Maafikiano ya Sochi" yatabainishwa na kujadiliwa katika kikao cha pande tatu cha mawaziri wa mambo ya nje wa Iran, Russia na Uturuki kitakachofanyika pembeni ya mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.../

Tags

Sep 19, 2018 14:18 UTC
Maoni