• Mazoezi ya pamoja ya anga ya SEPAH na Jeshi la Iran yaanza katika maji ya Ghuba ya Uajemi

Kaimu Mkuu wa Uenezi wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Kwa mnasaba wa kuanza Wiki ya Kujihami Kutakatifu mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya vikosi vya anga vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH (IRGC) na vya Jeshi yameanza katika maji ya Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman.

Kanali Yosef Safiy Pur amewaeleza waandishi wa habari pembeni ya mazoezi hayo ya kijeshi kwamba: Ndege tisa za kivita aina ya F4, ndege nne aina ya Mirage, ndege sita aina ya Sukhoi 22, ndege nne aina ya Tucano, ndege tatu aina ya Yak-12, helikopta tatu aina ya Chinook na helikopta mbili aina ya 212 zinashiriki kwenye mazoezi hayo.

Mbali na kubainisha kwamba manuva ya pamoja ya vikosi vya anga vya SEPAH na Jeshi ni kielelezo cha nguvu na ujumbe wa amani na urafiki kwa nchi rafiki na jirani, Kanali Safiy Pur amesema: Endapo maadui wataingiwa na tamaa, wakajaribu kufanya uchokozi wowote dhidi ya Iran ya Kiislamu watakabiliwa na jibu la kipigo kali.

Mazoezi ya kivita ya jeshi la majini la Iran

Katika kalenda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tarehe 31 Shahrivar inayosadifiana na tarehe 22 Septemba ni siku vilipoanza vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran, ambapo huanza maadhimisho yaliyopewa jina la Wiki ya Kujihami Kutakatifu.

Maadhimisho ya mwaka wa 38 wa Wiki ya Kujihami Kutakatifu yataanza rasmi hapo kesho na kuendelea kwa muda wa wiki moja nchini kote.

Itakumbukwa kuwa katika vita vya miaka minane dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, jeshi la utawala wa Baathi wa Saddam liliungwa mkono kwa hali na mali na madola ya kiistikbari na kupatiwa misaada chungu nzima na nchi za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi. Hata hivyo licha ya mbinyo na vizuizi vya kila upande, Iran iliweza kwa azma thabiti kusimama imara na kukabiliana na ubabe na utumiaji mabavu wa madola makubwa ya dunia yaliyokuwa yakiuunga mkono utawala vamizi wa Saddam.../  

Tags

Sep 21, 2018 07:46 UTC
Maoni