• Rouhani: Taifa la Iran kwa mara nyingine litawakatisha tamaa maadui

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema taifa la Iran, sawa na miaka ya huko nyuma litakatisha tamaa na kumvunja moyo adui na kuongeza kuwa: Leo hakuna tena vita vya niaba bali Marekani imeingia katika medani kupambana moja kwa moja na taifa la Iran na inavunja ahadi zake.

Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo asubuhi mjini Tehran katika gwaride ya majeshi ya Iran na kuashiria hatua ya Marekani kuvunja ahadi zake kwa kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji, JCPOA. Rais wa Iran ameongeza kuwa: "Donald Trump amejiondoa kidhahiri katika JCPOA lakini lengo lake kuu ni kutoa pigo kwa Mapinduzi na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."

Rais Rouhani ameashiria vita vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya Iran na kusema: "Walimwengu leo wanalaani hatua ya Marekani na bila shaka Marekani ndio itakayoshidnwa na kupata pigo katika vita hivi vya kiuchumi, kisaikolojia na kisiasa."

Ameendelea kusema kuwa, taifa la Iran leo linapendwa na watu wa Iraq, Syria na Lebanon na kuongeza kuwa: "Taifa la Iran halitalegeza msimamo kuhusiana na uwezo wake wa kujihami hasa uwezo wa makombora bali hata litazidi kuimarisha uwezo wake wa kujihami."

Gwaride ya Majeshi ya Iran, Tehran 22/09/2018

Akiashiria ushawishi wa Iran katika eneo, Rais Rouhani amesema: "Kwa muda mrefu Iran imekuwa ikilinda na kudhamini usalama wa Ghuba ya Uajemi, Bahari ya Hindi na Lango Bahari la Babul Mandab na hivyo ikiwa kama nchi kubwa na yenye ushawishi Mashariki ya Kati haitanyamaza kimya wakati mataifa mengine yanapodhulumiwa."

Rais wa Iran ameashiria pia vita vya kulazimishwa vya utawala ulioanguishwa ba Baath wa Iraq dhidi ya Iran kuanzia mwaka 1980 hadi 1988 na kusema: "Pamoja na jinai zote za kivita na uvamizi uliotekelezwa na utawala wa Saddam dhidi ya Iran, hakuna dola lolote kubwa wala hakuna shirika lolote la kimataifa lililosimama kuzuia uvamizi huo na hilo lilikuwa somo kubwa kwa Iran."

Tags

Sep 22, 2018 07:10 UTC
Maoni