Sep 22, 2018 12:07 UTC
  • Wiki ya Kujitetea Kutakatifu; katika mwaka wa 40 wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu

Katika kalenda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tarehe 31 Shahrivar ambayo ni sawa na tarehe 22 Septemba na inayosadifiana na kuanza vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran, imetajwa kuwa mwanzo wa Wiki ya Kujitetea Kutakatifu.

Miaka minane ya vita vya kujitetea kutakatifu, inakumbusha ukakamavu wa taifa la Iran ambalo kutokana na utamaduni wake wa Ashura, liliweza kusimama imara mbele ya uistikbari wa dunia na washirika wake na huku likiwa mikono mitupu ama likitegemea wananchi wake wanaotii viongozi wao wa kidini, liliuthibitishia ulimwengu kwamba uhuru na utukufu unapatikana katika mapambano. Akizungumza hivi karibuni mbele ya umati mkubwa wa makamanda, mashujaa wa vita, wasanii na wasimamizi wa vipindi vya Nyusiku Zinazokumbusha Kujitetea Kutakatifu, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisisitiza kwamba licha ya kupatikana hasara za kiroho na kimaada, lakini kipindi cha Kujitetea Kutakatifu kilikuwa na taathira muhimu kwa ajili ya kizazi cha leo na cha kesho. Alisisitiza kwamba kulindwa na kuimarishwa moyo wa kimapinduzi katika jamii na kudumu kwa mapinduzi hayo ni moja ya taathira hizo za kipindi cha Kujitetea Kutakatifu na kwamba kama isingelikuwa ni harakati hiyo ya kijihadi na ya kujitolea, bila shaka moyo wa kimapinduzi nchini ungekuwa hatarini.

Ayatullah Ali Khamenei akiwa mbele ya wanajeshi

Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kukaribia Wiki ya Kujitetea Kutakatifu limetoa taarifa likisema kuwa adui anapasa kufahamu vyema kuwa moyo wa Ashura wa wananchi wa Iran kamwe hautatoa mwanya wa kutwishwa taifa hili irada na matakwa batili na yasiyokubalika. Katika kipindi chote cha miaka minane ya Kujitetea Kutakatifu, Jamhuri ya Kiislamu ilijitahidi kuheshimu misingi ya maadili, sheria za kimataifa pamoja na maadili ya vita. Ama kwa upande wa pili utawala wa kijinai wa Saddam Hussein kwa miaka yote hiyo ulikiuka waziwazi sheria hizo za kimataifa na maadili ya vita. Mashambulio ya mara kwa mara ya silaha za kemikali, kuanzisha vita vya miji na mashambulio dhidi ya raia wa kawaida ni miongoni mwa vitendo vya ukiukaji wa maadili vilivyotekelezwa na utawala huo wa Kibaathi katika vita vyake vya kichokozi dhidi ya Iran na kwa msaada wa Marekani na dola za mafuta za baadhi ya nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaichukulia Marekani kuwa muhusika mkuu wa uvurugaji amani na usalama katika eneo, iwe ni katika kipindi cha vita vya kulazimishwa au hivi sasa. Watawala wa Marekani hawajagoma kufanya shari na kuanzisha migogoro katika eneo na wangali wanatekeleza njama kubwa kwa ajili ya kutoa pigo dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Moja ya makombora ya kujilinda ya Iran

Uzoefu wa kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu umethibitisha wazi kwamba ili kukabiliana na vitisho na kujilinda kutokana na ashari ya  wachokozi, nchi inapasa kujitayarisha katika pande zote. Kuhusu jambo hilo, Ismail Qadimi, mhadhiri wa masuala ya mawasiliano na uandishi wa magazeti anasema kwamba katika vita vya miaka minane, ni wazi kuwa Iran ilikuwa imejiandaa vyema katika upande wa kimaanawi, kibinadamu na uwekezaji wa kijamii na kiutamaduni kuliko Iraq, na muhimu kuliko yote, kiitikadi na uwezo wa kuwahamasisha wananchi wake. Anasema, hata hivyo vita hivyo kwa mara nyingine vilithibitisha wazi kwamba ubora wa teknolojia ni jambo lisilopingika katika ustawi na maendeleo na kwamba katika dunia ya leo ubora wa mwanadamu unapasa kwenda sambamba na ubora wa teknolojia.

Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama ulivyofanikiwa kusimama imara mbele ya adui mchokozi, leo pia umesimama imara katika mapambano yake dhidi ya ugaidi na magaidi katili wanaodhaminiwa na Marekani katika eneo, na wala haitatoa mwanya kwa madola ya kibeberu kudhoofisha nguvu ya kujidhaminia usalama wake na wa eneo zima la Mashariki ya Kati.

Maoni