Sep 22, 2018 16:52 UTC
  • Licha ya hujuma ya kigaidi mjini Ahvaz, gwaride la kufana lafanyika katika miji yote ya Iran

Licha ya shambulizi la kigaidi lililofanywa mjini Ahvaz, kusini magharibi mwa Iran, gwaride la kufana la majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa mnasaba wa kuanza Wiki ya Kujihami Kutakatifu, limefanyika katika miji yote nchini.

Asubuhi ya leo limefanyika gwaride kubwa la vikosi vya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na vikosi vya jeshi la kujitolea la wananchi la Basij na vikosi vya jeshi la Polisi katika mikoa na miji mbalimbali nchini. Katika gwaride hilo vikosi hivyo vya ulinzi, vikiandamana na silaha na zana mbalimbali za kijeshi  vimeonyesha utayarifu wao wa kiulinzi.

Hata hivyo katika gwaride lililofanyika mjini Ahvaz, kundi la kigaidi na ukufurishaji la al-Ahvaziyah linaloungwa mkono na Uingereza na Saudi Arabia na ambalo mwaka jana pia lilishambulia misafara ya watu wanaozuru maeneo ya kumbukumbu za vita, lilishambulia kwa risasi gwaride hilo kwa kuwalenga wananchi waliokuwa wakitazama maonyesho hayo ya kijeshi ambapo kutokana na shambulizi hilo watu kadhaa wasio na hatia wakiwemo wanawake na watoto wameuawa na kujeruhiwa.

Gwaride la vikosi vya ulinzi likitoa heshima mbele ya Rais Hassan Rouhani

Shambulizi la kigaidi dhidi ya wananchi waliokuwa wanatazama gwaride la majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Ahvaz, limeonyesha jinsi maadui walivyopoteza matumaini ya kuibua ghasia na machafuko ya mitaani nchini hapa katika mpango uliopewa jina la Msimu wa Joto Linalotokota, lakini kutokana na kugonga mwamba njama hiyo maadui wameamua kuanzisha tena mashambulio ya kigaidi ya kuua raia wa kawaida.

Wakati huohuo Naibu wa Mkuu wa Mkoa wa Khuzestan wa masuala ya kisiasa na kijamii amesema watu 25 wameuawa shahidi na wengine 60 wamejeruhiwa kutokana na shambulio la kigaidi lililofanywa leo mjini Ahvaz.

Ali Hossein Hosseinzadeh aidha amethibitisha kuwa magaidi wanne waliofanya shambulio hilo wameangamizwa.

Wakati huohuo Rais Hassan Rouhani amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri wa Mambo ya Ndani Abdoreza Rahmani Fazli na Mkuu wa Mkoa wa Khuzestan Gholamreza Shariati na kusisitiza kuchukuliwa hatuua kali kwa wahusika wa shambulio la kigaidi lililotokea mjini Ahvaz, mkoani Khozestan kusini magharibi mwa Iran.../

Tags

Maoni