• Sisitizo la Kiongozi Muadhamu la kusakwa na kukabidhiwa kwa vyombo vya sheria watenda jinai wa shambulio la kigaidi la Ahvaz

Tukio chungu na la kusikitisha la kuuawa shahidi wananchi kadhaa katika mji wa Ahvaz na magaidi mamluki, kwa mara nyingine tena limedhihirisha ukatili na ukhabithi wa maadui wa taifa la Iran.

Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Ahvaziya ambalo linaungwa mkono na Saudi Arabia na Uingereza jana Jumamosi lilishambulia kwa risasi kutoka katika bustani moja pambizoni mwa  gwaride majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa mnasaba wa kuanza Wiki ya Kujihami Kutakatifu mjini Ahvaz na kuwaua shahidi raia 25 na kuwajeruhi wengine 60 waliokuwa wakitazama gwaridwe hilo. Kufuatia shambulio hilo la kigaidi, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ametuma salamu za rambirambi kwa familia za mashahidi wa tukio hilo chungu na kusisitiza kwamba, vyombo husika vya intelejinsia vina wajibu wa kuhakikisha vinachukua hatua haraka na kwa umakini kuwasaka wahusika waliosalia wa jinai hiyo na kuwakabidhi mikononi mwa vyombo imara vya mahakama nchini. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika risala yake hiyo ya rambirambi kwamba: Mamluki hawa wenye nyoyo katili wanaowamiminia risasi wanawake, watoto wadogo na watu wasio na hatia ni vibaraka wa watu walewale waongo na wazandiki wanaojidai kila mara kuzungumzia haki za binadamu, wakati nyoyo zao zilizojaa chuki haziwezi kuvumilia kuona nguvu na uwezo wa kitaifa unaoonyeshwa na vikosi vya ulinzi vya Iran.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Swali la muhimu ambalo hujitokeza kila baada ya operesheni yoyote ya kigaidi ni hili kwamba, ni mtu au watu gani waliohusika na tukio hilo? Hapana shaka kuwa, nyuma ya pazia shambulio la kigaidi la Ahvaz ni zilezile harakati ambazo zimekuwa zikifanyika kwa uratibu wa Marekani na moja ya madola ya eneo yenye fikra mgando ambalo daima limekuwa likiunga mkono magaidi wa kitakfiri. Kundi hili mwaka uliopita pia lilishambulia watu wanaoshiriki katika misafara ya nuru (ya kutembelea maeneo ya vita vya miaka minane vya kijihami kutakatifu-kuanzia 1980 hadi 1988-wakati Iraq ilipoivamia Iran).

Kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuwa, haikubaliki hata kidogo kuona msemaji wa kundi la kigaidi la Ahvaziya akiruhusiwa kutangaza kuhusika kundi lake na shambulio hilo kupitia Kanali ya Televisheni yenye makao yake mjini London Uingereza. Daima Marekani na Saudi Arabia zimekuwa pamoja na utawala haramu wa Israel katika Mashariki ya Kati, ambapo kwa kuanzisha na kuunga mkono makundi ya kigaidi kidhahiri na kwa kificho, daima yamekuwa mbioni kutekeleza mipango yao michafu katika eneo. Mhimili huo hatari wa pande tatu yaani Marekani, Saudi Arabia na  utawala dhalimu wa Israel uumeligeuza eneo la Magharibi mwa Asia (Mashariki ya Kati) kuwa uwanja wa chokochoko za kiugaidi.

Kama alivyobainisha bayana Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika salamu zake za rambirambi ni kuwa, jinai za kundi la al-Ahvaziya ni muendelezo wa njama za madola vibaraka wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati ambayo lengo lao ni kuzusha machafuko na ukosefu wa amani nchini Iran.

Askari akimsaidia mtoto aliyejeruhiwa kwa risasi katika shambulio la kigaidi la Ahvaz

Hapana shaka kuwa, uwezo na nguvu za Mfumo wa Jamhuuri ya Kiislamu ni sababu kuu kabisa ya uadui wa Marekani dhidi ya taifa la Iran. Tukio la kigaidi la jana Jumamosi limetokea katika hali ambayo, kundi la kigaidi la Daesh na makundi mengine ya kigaidi na kitakfiri yamepata mapigo makubwa nchini Iraq na Syria. Hii leo makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Marekani mengi kati yao yamo katika orodha ya makundi ya kigaidi ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya nchi hiyo. Makundi hayo yamekuwa yakitekeleza jinai kwa urahisi kabisa na yamekuwa yakiendelea na jinai hizo bila wasiwasi. Katika hali ambayo, licha ya kuwa, Saudi Arabia imekuwa nyuma ya vitendo vya kigaidi na kufurutu ada, lakini Rais Donald Trump wa Marekani anajitokeza na kucheza mchezo wa kudansi na upanga na Mfalme wa Saudi Arabia. 

Robert Fantina mtafiti wa masuala ya haki za binadamu wa nchini Marekani anaashiria undumakuwili katika sera za haki za binadamu za Marekani na kusema kuwa, ..."Haki za binadamu za Marekani zina uhusiano wa moja kwa moja na pato la mafuta na vyanzo vya fedha, hivyo basi madhali maslahi ya kifedha ya Marekani yanadhaminiwa, nchini Marekani suala la haki za binadamu halina maana."

Miamala hii ya kindumakuwili ambayo imefungua njia ya harakati za makundi ya kufurutu ada daima imepelekelea kukaririwa vitendo hivyo vya kigaidi na madhali undumakuwili huu ungalipo, basi usalama wa mataifa na haki za binadamu zinatendelea kuwa wahanga wa uchu na tamaa za kisiasa na maslahi ya haramu ya madola makubwa ulimwenguni. Hata hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiwezi kuathiriwa na harakati kama hizo na katu haiwezi kutetereka katika siasa zake za kimsingi na itaendelea bila kusita na mapambano dhidi ya ugaidi kwa shabaha ya kuongeza usalama na uthabiti wa eneo la Mashariki ya Kati.

Sep 23, 2018 07:48 UTC
Maoni