• Umoja wa Mataifa walaani shambulizi la kigaidi la Ahvaz Iran

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres amelaani shambulio la kigaidi lililoua makumi ya watu kusini magharibi mwa Iran.

Kupitia msemaji wake, Stephane Dujarric, Katibu Mkuu wa UN ametoa mkono wa pole kwa serikali na taifa la Iran kufuatia hujuma hiyo, huku akituma risala za rambirambi kwa familia za wahanga wa shambulizi hilo la jana.

Kadhalika amewatakia afueni ya haraka majeruhi wa ukatili wa magaidi.

Wakati huohuo, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imeeleza kusikitishwa kwake na shambulizi hilo, ambalo halikuwasaza hata watoto wadogo na wanawake.

Nayo harakati ya muqawama ya Lebanon Hizbullah sambamba na kulaani hujuma hiyo, imesema shambulizi hilo ni radiamali ya maadui waliochukizwa na mafanikio ya harakati za mapambano katika eneo hili la Mashariki ya Kati.

Shambulizi la Ahvaz

Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani shambulio la kigaidi lililofanywa jana dhidi ya gwaride la vikosi vya ulinzi mjini Ahvaz kusini magharibi mwa nchi na kueleza kwamba: Iran inawabebesha dhima ya mashambulio ya aina hiyo waungaji mkono wa ugaidi katika eneo na bwana wao Marekani.

Watu wasiopungua 25 waliuawa shahidi na wengine 60 kujeruhiwa kutokana na shambulio la kigaidi lililofanywa jana mjini Ahvaz katika mkoa wa Khuzestan kusini magharibi mwa nchi, na kundi moja la kigaidi lililotangaza kuwa na mfungamano na Saudi Arabia.

Tags

Sep 23, 2018 07:50 UTC
Maoni