• EU wakataa kulaani shambulizi ya kigaidi Ahvaz, Iran

Umoja wa Ulaya haukulaani shambulizi la kigaidi lililofanyika katika mji wa Ahvaz nchini Iran na umetosheka tu kwa kutuma salamu za rambirambi kwa familia zilizopatwa na msiba na Wairani kwa ujumla.

Taarifa ya Umoja wa Ulaya iliyotolewa jana Jumapili imesema kuwa: Jumamosi iliyopita watu 25 waliuawa katika shambulizi la kigaidi lililolenga gwaride la jeshi katika mji wa Ahvaz na makumi ya wengine wamejeruhiwa. 

Kitendo cha Umoja wa Ulaya cha kutolaani shambulizi la kigaidi la Ahvaz nchini Iran ni ishara ya siasa za kindumakuwili za nchi za Magharibi kuhusiana na ugaidi.

Vyombo vya habari vya nchi hizo kama New York Times, Washington Post, The Huffington Post na mashirika ya habari ya Ufaransa na Reuteres pia yamejiepusha kuyataja mashambulizi ya Jumamosi iliyopita mjini Ahvaz kuwa ni ya kigaidi. 

Hii ni licha ya kwamba, vyombo vya habari vya nchi za Magharibi hulivalia njunga tukio lolote dogo linalojiri katika nchi za Ulaya na Marekani kama mapigano yanayoshirikisha silaha baridi kama kisu na nyundo na kuyapa "sifa na majina ya ugaidi".

Askari wa Iran akiokoa raia, Ahvaz

Makundi ya kigaidi ya DAESH na Al Ahvaziyyah yanayoungwa mkono na Saudi Arabia na Marekani yametangaza kuwa wanachama wao walishiriki kwenye shambulio la kigaidi la Ahvaz.

Watu 25 waliuawa shahidi na wengine zaidi ya 60 walijeruhiwa katika shambulio la kinyama la kigaidi lililofanywa asubuhi ya Jumamosi mjini Ahvaz, ambapo magaidi wenye silaha waliwafyatulia risasi wananchi waliokuwa wakitazama gwaride la vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mnasaba wa maadhimisho ya Wiki ya Kujihami Kutakatifu.

Sep 24, 2018 06:46 UTC
Maoni