Sep 24, 2018 12:45 UTC
  • Safari ya Rais wa Iran mjini New York; fursa ya kubainisha changamoto za kieneo na kimataifa

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana Jumapili aliekekea New York Marekani kwa lengo la kushiriki mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Kushiriki katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni fursa kwa nchi zinazohudhuria mkutano huo katika uga wa kisiasa na ushirikiano wa kimataifa. Fursa hiyo ina umuhimu pia kwa Iran kwa shabaha ya kubainisha mitazamo na misimamo yake kuhusu masuala mbalimbali ya dunia. Safari hiyo inaweza kuzingatiwa katika pande mbili muhimu na moja ya pande hizo ni mjadala kuhusu ugaidi ambapo Iran ni miongoni mwa nchi wahanga na zilizoathiriwa na  ugaidi unaoungwa mkono na nchi za Magharibi na waitifaki wao katika eneo la Mashariki ya Kati. Nukta ya pili ambayo ina uhusiano na ile ya kwanza, ni suala la amani na usalama duniani hususan katika eneo la Asia Magharibi. 

Jumamosi iliyopita ya tarehe 22 Septemba wakati wa shambulio la kigaidi lililofanywa katika mji wa Ahvaz nchini Iran ulimwengu ulishuhudia tena uhakika kwamba Iran ni miongoni mwa nchi wahanga wa ugaidui. Siasa za Marekani za kutumia ugaidi kama wenzo wa kutimizia malengo na matakwa yake na wakati huo huo kujitokeza makundi ya kigaidi katika maeneo mbalimbali duniani kunafanyika kwa lengo la kuzusha machafuko na kisha kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Nchi za Afghanistan, Iraq, Syria na Yemen kwa miaka kadhaa sasa zimegeuzwa maeneo ya kutekelezea siasa za kivamizi za Marekani, Israel na Saudi Arabia. Lengo la muungano huo vamizi ni kuanzisha vita na kueneza ugaidi na matokeo yake ni kuyasababishia mataifa mbalimbali hasara na maafa yasiyoweza kufidika. Wakati huo huo kadhia ya Palestina pia ni  jeraha la muda mrefu huku eneo la Ukanda wa Ghaza likiendelea kukabiliwa na  mashambulizi na hujuma mtawalia za utawala wa Kizayuni wa Israel. 

Wapalestina wa Ukanda wa Gaza wakikabiliana na mashambulizi ya wanajeshi wa Israel. 

Katika upande wa mahusiano ya kimataifa pia kunashuhudiwa changamoto nyingi ambazo chimbuko lake ni ubeberu na sera za kupenda kujitanua za Marekani. Miongoni mwa mifano ya changamoto hizo ni ni sera za Marekani za kutaka kuikwamisha Iran kupitia njia ya kukiuka na kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Marekani haikuweza kustahamili anga ya ushirikiano iliyojitokeza baada ya kufikiwa makubaliano hayo na inafanya jitihada kuvuruga anga hiyo na makubaliano hayo ya kimataifa yaliyoungwa mkono na kupasishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Marekani pia inavuruga bishara huru ya kimataifa kwa kutoa vitisho na kuziwekea vikwazo nchi nyingine, hatua ambayo haina manufaa ya nchi yoyote. 

Ni wazi kuwa Marekani inazusha hali ya machafuko katika eneo la Mashariki ya Kati kwa kuyaunga mkono makundi ya kigaidi lengo likiwa ni kuligawa eneo hili. Marekani inafanya hayo yote huku nchi za eneo hili zikihitaji kuwa na mifumo thabiti, usalama wa jamii, ustawi na ushiriki wa kiuchumi wenye tija. 

Katika mazingira kama hayo, kushiriki Rais wa Iran katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, kwa kuzingatia hali nyeti ya sasa katika Mashariki ya Kati, ni fursa nzuri kwa ajili ya kujadiliwa mienendo ya kiadui na kiuhasama ya Marekani katika kikao hicho cha kimataifa. Aidha walimwengu wanasubiri kusikia uwongo na bwabwaja za Trump na tawala zinazotenda jinai kama Israel na Saudi Arabia zinazotumia kila fursa ili kutoa pigo kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; na tawala hizo hivi sasa zimejikita katika suala la kushadidisha vita vya kisaikolojia dhidi ya Iran katika mkutano huo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. 

Rais Donald Trump wa Marekani 

Wananchi wa Iran mara kadhaa wamedhihirisha kuwa, si tishio kwa mataifa mengine na hawatetereshwi na vitisho vya mtu au nchi yoyote. Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameelekea New York kwa lengo la kubainisha misimamo ya wazi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu mustakbali wa mataifa ya ulimwengu na kwa shabaha ya kuondoa sintofahamu na propaganda zinazofanwya na maadui dhidi ya taifa la Iran. 

Maoni