Sep 24, 2018 15:26 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Tutatoa kipigo kikali kwa watu waoga waliohusika na tukio chungu la Ahvaz

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kuwashambulia watu wasio na ulinzi ni kitendo cha watu waoga na kusisitiza kwamba, hapana shaka kuwa, taifa hili litatoa jibu kali kwa wahusika wa tukio chungu la Ahvaz kusini magharibi mwa Iran.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo alipokutana na wanamichezo wa Kiirani waliotwaa medali katika mashindano ya michezo mbalimbali ya mataifa ya Asia ya mwaka huu yaliyofanyika Jakarta Indonesia ambapo ameashiria shambulio la kigaidi la siku ya Jumamosi mjini Ahvaz na kubainisha kwamba, kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, tukio hilo limefanywa na walewale watu waoga ambao kila mahala wanaponasa huko Iraq na Syria, Wamarekani huja na kuwaokoa, na fedha zao wanapata kutoka kwa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati).

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema bayana kwamba, tukio hili chungu kwa mara nyingine tena limeonyesha kuwa, taifa la Iran limo katika njia ya fakhari nyingi za ustawi na kukwea na lina maadui wengi.

Wanamichezo waliotwaa medali katika mashindano ya michezo  ya mataifa ya Asia wakimsikiliza Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu (24.09.2018)

Akibainisha sababu ya wanamichezo wa Iran kususia kukabiliana na wanamichezo wa utawala wa Kizayuni wa Israel,  Ayatullah Khamenei amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tangu mwanzoni mwa Mapinduzi, haikuutambua utawala ghasibu wa Israel na utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, tab'an utawala wa apartheid wa Afrika Kusini umeanguka na utawala ghasibu, muongo na wa kibaguzi wa Israel nao utaanguka na kusambaratika.

Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitakubali kupambana katika michezo na wanamichezo wa utawala ghasibu wa Israel, na kwamba inaamini kuwa, kitendo kilichofanywa mwaka jana na mwanamichezo Alireza Karimi cha kususia kushindana na mwanamichezo wa utawala haramu wa Israel ni mfano mmoja wa mwanamichezo ambaye ni bingwa halisi.

Maoni