Sep 25, 2018 02:25 UTC
  • Ali Shamkhani: Ugaidi ni kikwazo kikubwa katika njia ya ustawi wa nchi za Kiislamu

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, hatari ya ugaidi na mizizi yake ni miongoni mwa fikra za kitakfiri zinazoenezwa na baadhi ya nchi za Kiislamu katika Mashariki ya Kati ambazo zimelitumbukiza eneo lote hili katika mgogoro na kuwa kikwazo kikubwa katika njia ya ustawi na maendeleo ya nchi za Kiislamu.

Ali Shamkhani alisema hayo jana katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Ramil Usubov, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Azerbaijan ambapo amesema kuwa, siasa chafu na mbaya za Marekani na utawala dhalimu wa Israel zimekuwa zikizusha mifarakano baina ya nchi jirani.

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kuna ulazima wa kuwa macho, kuongeza ushirikiano na mazungumzo kwa shabaha ya kukwamisha na kusambaratisha njama haribifu za wale wenye kuyatakia mabaya mataifa ya Kiislamu na ambao wanafanya kila wawezalo ili kuleta mtazamo mbaya na kuzusha hitalafu baina ya nchi za eneo. 

Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran katika mazungumzo yake na Ramil Usubov, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Azerbaijan (24.09.2018)

Ali Shamkhani ameashiria kutokuwa halali vikwazo vya Marekani na kufanywa kuwa wenzo wa Rais Donald Trump wa kulipiza kisasi dhidi ya nchi zinazoipinga Washington na kuongeza kuwa, hatua hizo si tu kwamba, hazina taathira yoyote bali zitaifanya Marekani izidi kutengwa na jamii ya kimataifa.

Kwa upande wake, Ramil Usubov, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Azerbaijan sambamba na kulaani shambulio la kigaidi la Jumamosi mjini Ahvaz kusini magharibi mwa Iran amesema kuwa, kwa kuzingatia vitisho vya pamoja vya makundi ya kigaidi na kitakfiri, serikali ya Baku ina shauku ya kutumia uzoefu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kukabiliana na vitisho tarajiwa.

Tags

Maoni