Sep 25, 2018 03:02 UTC
  • Rais Rouhani: Ni mustahili kuizuia Iran kuuza mafuta yake

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amegusia njama za Marekani za kujaribu kuizuia Iran isiuze mafuta yake na kusisitiza kuwa, shabaha ya Wamarekani ya kuizuia Iran kuuza mafuta yake si tu ni jambo mustahili na lisilowezekana, lakini hata ni hatari sana.

Rais Rouhani amesema hayo mbele ya wakurugenzi wa ngazi za juu wa vyombo vya habari vya Marekani mjini New York na huku akimtaka rais wa nchi hiyo Donald Trump arekebishe vitendo vyake viovu mno dhidi ya taifa la Iran amesema, Trump amejitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kuanza kuliwekea vikwazo na kutoa vitisho dhidi ya taifa la Iran bila ya sababu yoyote mbali na kuingilia waziwazi masuala ya ndani ya Iran, hivyo, anapaswa kujirekebisha kwanza kabla ya jambo lolote lile.

Amesema, vikwazo vya Marekani dhidi ya wananchi wa Iran ni vya kidhalimu na ni kinyume cha sheria na bila ya shaka mtazamo wa wananchi wa Iran kuhusu Marekani hauwezi kuwa mzuri hata kidogo na ni kwa sababu hiyo pia ndio maana katika maandamano ya mamilioni ya watu, nara za wananchi wa Iran dhidi ya serikali ya Marekani zinazidi kuwa kali kuliko wakati mwingine wowote.

Rais Rouhani katika mahojiano na vyombo vya habari mjini New York Marekani alikokwenda kushiriki mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia pia pendekezo la mazungumzo lililotolewa na Marekani na kusisitiza kuwa, kama itatokezea siku, Marekani ikawa kweli ina nia njema, wakati huo ndipo Iran itaamua cha kufanya kuhusu mazungumzo.

Amezungumzia pia namna baadhi ya nchi zilizovyohusika katika shambulizi la kigaidi la Jumamosi wiki hii huko Ahvaz, kusini magharibi mwa Iran na kusema, tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hadi hivi sasa, Marekani imekuwa ikiyaunga mkono na kuyasaidia magenge ya kigaidi yanayofanya jinai nchini Iran.

Rais Hassan Rouhani yuko mjini New York Marekani kwa ajili ya kushiriki katika mkutano wa 73 wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Tags

Maoni