Oct 16, 2018 15:57 UTC
  • Rais Rouhani: Kuimarisha uhusiano na nchi za bara la Afrika ni miongoni mwa sera za Iran

Rais Hassan Rouhani amesema kustawisha na kuimarisha uhusiano na nchi za bara la Afrika ikiwemo Senegal ni miongoni mwa sera za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akasisitiza kwamba Tehran iko tayari kupanua uhusiano wake na Dakar katika nyanja zote.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo baada ya kupokea hati za utambulisho za balozi mpya wa Senegal mjini Tehran, Amadou Sow. Rais Rouhani amebainisha kuwa, kuimarisha uhusiano na Senegal ambayo ni nchi rafiki na ya Kiislamu kumekuwa kukipewa umuhimu kila mara na Iran na akaeleza matumaini aliyonayo ya kupanuliwa zaidi uhusiano huo wa kirafiki na kiudugu kutokana na irada na azma ziliyonayo serikali za nchi mbili.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekaribisha pia uamuzi wa kurahisisha utoaji viza ya kuingia Senegal kwa wafanyabiashara wa Iran na akaeleza kwamba: Mashirika ya Iran yako tayari kupanua zaidi shughuli zao katika sekta za ujenzi, uundaji magari, utengezaji dawa na utoaji huduma za afya nchini Senegal.

Rais Rouhani akikagua hati za utambulisho za balozi mpya wa Senegal

Rais Rouhani vilevile ameashiria udharura wa nchi zote kupambana na ugaidi barani Afrika na Mashariki ya Kati na akaeleza kwamba Iran iko tayari kupanua ushirikiano wake na Senegal katika kupambana na ugaidi.

Baada ya kukabidhi hati zake za utambulisho, balozi mpya wa Senegal mjini Tehran amesema, nchi yake imedhamiria kuimarisha zaidi uhusiano wake na Iran katika nyanja zote hususan ya uchumi.

Amadou Sow ameeleza kwamba, Senegal inaweza kuwa njia ya kuingizia bidhaa za Iran magharibi mwa Afrika na akaongeza kuwa, Senegal aidha inataka kuwa na ushirikiano mpana na Iran katika mkakati wa kukabiliana na kupambana na ugaidi.../

Maoni