Oct 23, 2018 07:42 UTC
  • Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran na jukumu la Ulaya la kukabiliana na hatua za upande mmoja na sheria za nje ya mipaka za Marekani

Iran imeunga mkono na kukaribisha irada ya Ufaransa ya kukabiliana na hatua za upande mmoja na sheria za nje ya mipaka za Marekani.

Sayyid Abbas Araqchi Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia masuala ya kisiasa amekutana na kufanya mazungumzo hapa Tehran na Philippe Bonnecarrere Mkuu wa Kundi la Urafiki wa Kibunge kati ya Ufaransa na Iran katika bunge la seneti la Ufaransa na Delphine O Mkuu wa Kundi la Urafiki wa Kibunge  kati ya Ufaransa na Iran katika bunge la taifa la Ufaransa na kusisitiza kwamba: Jitihada zinazofanywa na Ulaya kuhusu makubaliano ya JCPOA zinapaswa kupelekea kupatikana ufumbuzi wa kiutekelezaji na kioparesheni.  

Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa 

Duru ya pili ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran itaanza kutekelezwa tarehe nne mwezi ujao wa Novemba kwa kujikita katika uuzaji nje mafuta ya Iran. Kuurejesha hadi sifuri uuzaji huo wa mafuta ya Iran nje ya nchi ndio lengo kuu zaidi la Trump katika marhala hii ya vikwazo; hata hivyo ushahidi unaonyesha kuwa hakuna njia iliyoandaliwa ili kufikiwa lengo hilo na nchi za Ulaya zinataraji kuchukua uamuzi wa kukabiliana na kusimama kidete dhidi ya  hatua hizo za upande mmoja za Marekani. Jarida la Foreign Affairs lenye mfungamano na Baraza la Uhusiano wa Nje la Marekani limeandika makala kuwa: Kitendo cha Marekani kudhani kuwa inaweza kutoa pigo kwa uchumi wa Iran kwa kukata uuzaji wake wa mafuta nje ya nchi kimegonga mwamba. 

Nchi za Ulaya zinafanya jitihada hadi kabla ya tarehe nne Novemba ziwe zimekwisha andaa mfumo wa kiutendaji wa kuunga mkono makubaliano hayo ya nyuklia. Kikao kilichofanyika mwezi uliopita pambizoni mwa Mkutano wa  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York chini ya uwenyekiti wa Bi Federica Mogherini Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya na kuhudhuriwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na kundi la 4 +1 kilitoa taarifa yake ya pamoja kuhusiana na suala hilo. Katika kikao hicho, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa kundi la 4+1 walikaribisha mapendekezo ya kivitendo kwa ajili ya kulinda na kustawisha mifumo ya ulipaji pesa na hasa juu ya kuanzisha taasisi ya mfumo maalumu utakaorahisisha miamala ya kifedha inayohusiana na uuzaji nje na uagizaji bidhaa wa Iran, yakiwemo mafuta.  

Akitilia mkazo kuendelea mchakat huo, Philippe Bonnecarrere Mkuu wa kundi la Urafiki wa Kibunge kati ya Ufaransa na Iran katika bunge la seneti la Ufaransa amesisitiza katika mkutano na waandishi habari hapa Tehran kuwa nchi za Ulaya zinafanya juhudi za kulinda makubaliano hayo ya nyuklia. Afisa huyo wa bunge la Ufaransa amesema: Tunafanya juhudi hadi kufikia tarehe nne Novemba mwezi huu tuwe tumeunganisha kwa uchache benki moja ya Iran na Swift yaani mfumo wa mawasiliano ya kifedha wa kimataifa na kwa njia hiyo kuendeleza miamala ya kibenki na kifedha na Iran kwa ajili ya bidhaa na huduma ambazo hazijajumuishwa ndani ya vikwazo. 

Kuna udharura wa kupatikana mfumo maalumu wa kutekeleza miamala ya kibenki itakayoifanya Iran inufaike na JCPOA na Ufaransa inafanya kila inaloweza kufuatilia mchakato huo kwa kustafidi na mifumo ya kuyalinda makubaliano hayo. Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mwezi Septemba mwaka huu alifanya mazungumzo ya simu na Rais wa Ufaransa na kueleza kuwa: Iwapo Ulaya haitatekeleza ahadi na majukumu yake sisi pia tutafuata njia ya tatu kuhusiana makubaliano ya JCPOA.  

Rais Hassan Rouhani aliyefanya mazungumzo ya simu na Rais wa Ufaransa kuhusu JCPOA
Maoni