Nov 12, 2018 15:12 UTC
  • Jeshi la Iran kulinda meli za mafuta baada ya vitisho vya Marekani

Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limetangaza azma yake ya kulinda meli za mafuta za nchi hii kutokana na vitisho vya Marekani vya kuzizuia.

Katika taarifa Admeli Mahmoud Mousavi, Naibu Kamanda wa Jeshi la Iran amesema leo Jumatatu kuwa: "Jeshi la Iran liko tayari, kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, kulinda meli zetu za mafuta kutokana na vitisho vyovyote."

Kauli hiyo imekuja bada ya Brian Hook mwakilishi maalumu wa Marekani kuhusu Iran kuwaonya washirika wa kibiashara wa Iran na kuwataka kutafakari upya kuhusu uamuzi wao wa kunuanua mafuta ya nchi hii kufuatia vikwazo vilivyowekwa na Marekani.

Akijibu vitisho hivyo, Mousavi ametahadharisha kuwa, hatua yoyote ya kuzuia meli za Iran katika maji ya kimataifa haikubaliki na kuongeza kuwa, majeshi ya Iran yako tayari kulinda meli za kibiasahra za nchi hii.

Tarehe 8 Mei mwaka huu, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kujitoa nchi yake kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kurejesha tena vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran. Awamu ya kwanza ya vikwazo hivyo ilianza kutekelezwa tarehe 7 Agosti na awamu ya pili ilianza kutekelezwa rasmi Jumatatu ya tarehe 5 Novemba.

Tags

Maoni