Nov 13, 2018 08:23 UTC
  • Zarif: Iran inajua mpango wa Saudia wa kufanya mauaji ya kigaidi dhidi ya maafisa wa ngazi za juu wa Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa Iran ikuwa na habari kuhusu mpango wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia wa kutaka kufanya mauaji ya kigaidi dhidi ya baadhi ya maafisa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu.

Dakta Muhammad Javad Zarif ameyasema hayo katika mahojiano yake na gazeti la al-Araby al-Jadeed linalochapishwa mjini London, Uingereza na kusisitiza kuwa Tehran ilikuwa na habari za uhakika kuhusu njama hiyo ya serikari ya Riyadh.

Matamshi hayo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran yametolewa baada ya gazeti la The New York Times la Marekani kufichua kwamba, mwezi Machi mwaka 2017 maafisa wa Saudi Arabia walikutana mjini Riyadh na kupanga njama ya kufanya mauaji dhidi ya maafisa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiwemo Meja Jererali Qassem Sulaimani.

Ripoti ya New York Times imesema kuwa mkutano huo pia uliwajumuisha wafanyabiashara kadhaa waliosuka mpango wenye thamani ya dola bilioni mbili na kutumia makampuni binafsi kwa ajili ya kuharibu uchumi wa Iran.

New York Times imefichua kwamba, njama hiyo ilipangwa wakati Mwanamfalme Mohammed bin Salman alipokuwa akiimarisha nguvu zake nchini Saudi Arabia na kwamba wakati huo pia ndipo ilipowekwa mipango ya kuwamaliza wapinzani wa utawala wa kifalme wa Saudia kama Jamal Khashoggi aliyeuawa zaidi ya mwezi mmoja uliopita katika ubalozi wa nchi hiyo mjini Istanbul Uturuki.

Tags

Maoni