Dec 08, 2018 15:34 UTC
  • Wazayuni, Wamarekani waunga mkono ugaidi nchini Iran

Waziri wa Usalama wa Taifa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel na mashirika ya kijasusi ya baadhi ya nchi za eneo ni waungaji mkono wa ugaidi ndnai ya Iran."

Sayyid Mahmoud Alawi Waziri wa Usalama wa Taifa ameyasema hayo leo pambizoni mwa Kongamano la Pili la Maspika wa Mabunge ya nchi za Kanda Kwa lengo la Kujadilia Vita Dhidi ya Ugaidi. Ameongeza kuwa, kwa mtazamo wa Marekani na Israel ugaidi unaotumiwa kufikia malengo yao si ugaidi.

Waziri wa Usalama wa Iran ameendelea kusema kuwa, Marekani hivi sasa inatuma magaidi wa ISIS au Daesh katika maeneo mbali mbali duniani.

Aidha amesisitiza kuwa, serikali za eneo zinapaswa kuhakikisha kuwa hakuna mazingiro ya kuibuka makundi ya kigaidi.

Rais Hassan Rouhani (katikati) na maspika wa mabunge ya nchi sita zilizoshiriki mkutano wa Tehran, 08,12,2018

Akizungumza katika kikao hicho, Spika wa Bunge la Iran, Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Ali Larijani amesema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halitekelezi majukumu yake katika kupambana na ugaidi.

Larijani amesema, hatua za upande moja ambazo zimechukuliwa na Rais Donald Trump wa Marekani ni hatari na zimezifanya kuwa za kibiashara haki za binadamu na thamani za kibinadamu ambazo zimechukua muda mrefu kustawi. Amesema pamoja na madai yake ya kupambana na ugaidi, Marekani na waitifaki wake wanaeneza ugaidi katika eneo hili. Ali Larijani amesema, lengo la kongamano la Tehran ni kuimarisha ushirikiano wa kiusalama baina ya wanachama na pia kuimarisha uhusiano wa kiuchumi ili kuboresha mshikamano wa kieneo.

Mkutano huo wa Tehran umefunguliwa mapema leo asubuhi kwa hotuba ya Rais Hassan Rouhani wa Iran na kuhudhuriwa na maspika wa mabunge ya Iran, China, Russia, Uturuki, Pakistan na Afghanistan.

Tags

Maoni