Dec 09, 2018 07:29 UTC
  • Jeshi la Majini la Iran kufanya mazoezi makubwa Bahari ya Hindi

Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran linapanga kufanya mazoezi makubwa katika Bahari ya Hindi kwa lengo la kujiimarisha na kuonyesha uwezo mkubwa wa kijeshi wa nchi hii.

Hayo yalidokezwa na Naibu Kamanda wa Jeshi la Majini la Iran anayesimamia uratibu Admeri Hamzeh Ali Kaviani Jumamosi jana. Ameongeza kuwa maneva hiyo itafanyika katika msimu ujao wa baridi ndani ya maji ya Iran kusini mwa nchi na pia katika maji ya kimataifa.
Amesema zana za kisasa zitakazotumika katika mazoezi hayo ni pamoja na nyambizi mbili za kiwango cha Ghadir ambazo karibuni hivi zilianza kutumika katika Jeshi la Majini la Iran. Nyambizi hizo zina uwezo wa kurusha makombora zikiwa ndani ya maji ya bahari na zilianza kutumika Novemba 29. Admeri Kaviani ameongeza kuwa, meli kadhaa za kivita, ikiwemo ile ya Sahand zitashiriki katika mazoezi hayo.

Meli ya kivita ya Iran ikijitayarisha kuelekea baharini kulinda doria

Meli hiyo ya kijeshi iliyoundwa kwa teknolojia na wataalamu wa hapa nchini, imesheheni mifumo ya kisasa yenye uwezo wa kuvurumisha makombora ya chini ya maji (torpedo) na ilizinduliwa mapema mwezi huu.
Manowari hiyo iliyopewa jina la Sahand ina uwezo wa kufanya operesheni za masafa marefu katika bahari kuu na kwa zaidi ya miezi miwili.
Jeshi la Majini la Iran mbali na kulinda maji ya taifa hili, lakini pia limezima mara kadhaa mashambulizi ya maharamia dhidi ya meli za mizigo na mafuta za nchi hii na nchi nyingine katika maji ya kimataifa.

Maoni