Dec 09, 2018 08:42 UTC
  • Taarifa ya Mkutano wa Tehran; sisitizo la ushirikiano wa kieneo wa kupambana na vitisho vya pamoja + Video

Jana Jumamosi, Tehran ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa Pili wa Maspika wa Mabunge ya Nchi Sita za Asia ambao ajenda yake kuu ilikuwa ni kuzuia na kupambana na ugaidi na misimamo mikali.

Maspika wa mabunge ya nchi sita za Iran, Afghanistan, Pakistan, Uturuki, China na Russia ulimalizika hiyo jana hapa mjini Tehran kwa taarifa ya pamoja ya kuimarisha uhusiano katika kupambana na ugaidi na kupanua wigo wa ushirikiano wa kieneo. 

Taarifa ya mwisho ya mkutano huo aidha imetangaza wazi wasiwasi wa nchi zilizoshiriki kwenye mkutano huo kuhusu hatari na athari mbaya za ugaidi kwa amani, usalama na maendeleo na kuhimiza wajibu wa kuchukuliwa hatua kali za kung'oa kabisa mizizi ya vitendo vyote vya kigaidi katika eneo hili sambamba na kuweka pembeni siasa za kindumilakuwili katika kupambana na ugaidi.

 

Nchi hizo sita zilizoshiriki kwenye mkutano huo wa jana hapa mjini Tehran kila moja kwa upande wake imepata madhara ya ugaidi. Wakati huo huo lakini, kila moja ya nchi hizo ina uzoefu na tajiriba nzuri ya ushirikiano katika kupambana na ugaidi, suala ambalo bila ya shaka yoyote lina umuhimu mkubwa katika vita dhidi ya ugaidi. 

Mashambulio ya kigaidi katika nchi za Iran, Afghanistan, Pakistan, Uturuki, China na Russia ni uthibitisho wa wazi wa kwamba nchi hizo zote zinaunganishwa katika udharura wa kushirikiana kupambana na hatari zao za pamoja. Mkutano wa jana wa Tehran ilikuwa ni fursa nzuri ya kujadiliwa mambo mengi katika uchanjaa huo. Amma kitu kilichojionesha kwa uwazi zaidi katika mambo yaliyozungumzwa kwenye mkutano huo wa Tehran ni kwamba nchi zote sita zina nia ya kweli ya kushirikiana katika masuala mbalimbali kama vile kuanzisha mfumo maalumu wa kubadilishana taarifa katika vita dhidi ya ugaidi na misimamo mikali.

Eneo hili hivi sasa linakabiliwa na hatari mbili kuu; ugaidi na magendo ya mihadarati ambayo ndiyo njia kuu inayotumika kuyadhaminia fedha magenge ya kigaidi hususan huko Afghanistan na Pakistan na matokeo yake ni athari mbaya kwa nchi zinazopakana na nchi hizo mbili. Ni kwa sababu hiyo ndio maana sisitizo kuu la washiriki wa mkutano wa jana wa Tehran likawa ni kufanyika jitihada za pande zote za kuleta amani na utulivu nchini Afghanistan kwani vitendo vya kigaidi na magendo ya madawa ya kulevya nchini humo vinazitumbukiza kwenye dimbwi la matatizo nchi zote zinazopakana nayo, kutaka na kukataa. 

 

Marekani na baadhi ya nchi ambazo zinajilabu kuwa ni viranja wa kupambana na ugaidi hazina mwamana kabisa na zinatumia ugaidi kama kiboko cha kuzichapa na kuzishinikiza nchi nyingine. Ni kwa sababu hiyo ndio maana nchi za eneo hili zikaamua kuwa na mfumo wao maalumu wa ushirikiano katika vita dhidi ya ugaidi na magendo ya mihadarati. Matunda ya ushirikiano kama huo wa kieneo yameonekana kwenye ushirikiano baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Uturuki na Russia katika utatuzi wa mgogoro wa Syria. 

Kwa upande wake, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika ufunguzi wa mkutano huo wa jana wa maspika wa mabunge ya nchi sita za Iran, Afghanistan, Pakistan, Uturuki, China na Russia kwamba, Iran ambayo ni muhanga mkubwa zaidi wa ugaidi iko tayari kushiriki vilivyo katika kulifanya eneo hili kuwa imara na madhubuti.

Katika ufunguzi wa mkutano huo, Rais Rouhani alitoa mapendekezo manane ya kufanyiwa kazi ambayo ni pamoja na kuimarishwa ushirikiano wa pande mbili na pande kadhaa; kuweko uratibu wa pamoja wa masuala ya usalama baina ya nchi zote jirani; kushiriki vilivyo katika jitihada za kuleta amani katika eneo hili; kutiwa nguvu kadiri inavyowezekana uwezo wa kiulinzi pamoja na kuweko ushirikiano wa pande kadhaa wa kidiplomasia na mikataba ya kibiashara.

 

Kwa upande wake, Lee Hian, mtaalamu na mchambuzi wa masuala ya vyombo vya habari kutoka China amesema kuwa, Iran ina nafasi bora na muhimu kabisa katika vita dhidi ya ugaidi katika eneo hili.

Amesema, ugaidi ni hatari kwa nchi zote za eneo hili na huku akiashiria juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kuleta usalama, utulivu na amani katika eneo hili ameongeza kuwa: Kama vita dhidi ya ugaidi vitadhoofika, basi nchi mbalimbali za dunia zitakuwa katika hatari ya kukumbwa na ugaidi. 

Ukweli wa mambo ni kuwa suala la usalama sasa hivi limechukua wigo mpana zaidi kuliko huko nyuma. Hivyo tunaweza kusema kuwa mikakati iliyowekwa na maspika wa mabunge ya Iran, Afghanistan, Pakistan, Uturuki, China na Russia katika mkutano wao wa jana wa Tehran inatoa dhamana ya kulindwa usalama wa nchi zote zilizoshiriki kwenye mkutano huo.

Maoni