Dec 11, 2018 15:57 UTC
  • Rouhani: Iran inaendelea kuuza mafuta yake duniani hata baada ya vikwazo vya Marekani

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema uuzaji mafuta ghafi ya petroli ya Iran katika soko la dunia unaendelea hata baada ya kuanza kutekelezwa awamu ya pili ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ambavyo vilianza Novemba Nne.

Hassan Rouhani, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo Jumanne mjini Tehran baada ya kumalizika kikao cha wakuu wa mihimili mitatu ya dola. Ameongeza kuwa: "Baada ya Nne Novemba, siku ambayo Wamarekani walikuwa wanaisubiri sana kuona uchumi wa Iran ukisambaratika, wananchi na wadau wa uchumi wamechukua hatua ambazo sasa zimeifanya Marekani ipate hasara."

Rais Rouhani ameendelea kusema kuwa: "Baada ya kutekelezwa duru ya pili ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, Wamarekani walijaribu sana kuona kunajiri mfumuko wa bei, matatizo ya kiuchumi na kuvurugika masoko ya Iran lakini kwa kuzingatia utendaji wa Benki Kuu ya Iran, wasimamizi wa uchumi na wananchi, utulivu umepatikana na jitihada zote sasa zinafanyika ili kudumisha utulivu huu na kupunguza matatizo ya wananchi."

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameendelea kubainisha kuwa, mchakato wa uuzaji nje bidhaa za Iran umekuwa mzuri katika kipindi cha miezi 8 iliyopita na ikilinganishwa na mwaka jana, kumekuwepo ongezeko la asilimia 13. Amesema Marekani imefeli katika vikwazo vyake vya mafuta dhidi ya Iran na kuongeza kuwa, "katika kikao cha OPEC, Marekani ilizishinikiza nchi wanachama zisipunguze uzalishaji lakini nchi za OPEC zimeamua kupunguza uzalishaji."

Akiashiria hali ya mambo katika eneo la Mashariki ya Kati, Rais Rouhani amesema kuwa, hali ya Yemen sasa imewalazimisha wavamizi wa nchi hiyo kuhisi kuwa hakuna njia nyingine isipokuwa kufikia mapatano ya amani na Wayemeni.

Kuhusu hali ya mambo nchini Syria, Rais Rouhani amesema nchi hiyo sasa inaelekea katika mkondo wa amani na hilo linamaanisha kufanikiwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tags

Maoni