Dec 13, 2018 07:21 UTC
  • Mike Pompeo
    Mike Pompeo

Sambamba na kutimia miaka 40 tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, uhasama na uadui wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu umefikia kileleni.

Katika siku hizi maafisa wa serikali ya Marekani wameshupalia kadhia ya makombora ya Iran na ushawishi wa Jamhuri ya Kiislamu katika eneo la magharibi mwa Asia na wamekuwa wakitumia majukwaa mbalimbali kuchochea fikra za walimwengu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Sera hizo zimekwenda sambamba na vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Iran baada ya kufeli siasa na vikwazo vya awali vya serikali ya Washington.

Kushupalia suala hilo la makombora ya Iran ambalo halikuashiriwa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA wala halina mfungamano wowote na nchi nyingine ni ishara ya kufeli kwa siasa na sera za Marekani katika jitihada zake za kuzichochea nchi nyingine dhidi ya Iran. Kushindwa huko kunaendelea kwa kipindi chote cha maia 40 iliyopita suala ambalo inaonekana ndilo sababu ya makelele ya sasa ya maafisa wa seikali ya Marekani. 

Miradi ya kuzalisha zana za kujihami ya Iran ni suala la ndani na kila nchi ina haki ya kufanya jitihada za kuimarisha nguzo zake za ulinzi na kujihami kwa mujibu wa ilani na stratijia zake za ulinzi. Katika mkondo huo huo kufanya majaribio ya makombora ni sehemu ya mikakati ya ulinzi ya kila nchi, na Iran imekuwa ikifanya majaribio kama hayo kulingana na mipango yake ya kuimarisha uwezo wa kukabiliana na mashambulizi yoyote ya adui. Hivyo hapana shaka kuwa, hatua ya maafisa wa serikali ya Marekani ya kuvalia njuga suala hilo ni kuingilia mambo ya ndani ya Iran, na pili ni kuendeleza propaganda chafu za kutaka kuidhihirisha Jamhuri ya Kiislamu kuwa ni tishio kwa nchi nyingine. 

Rais Donald Trump wa Marekani

Katika fremu hiyo, Jumanne iliyopita na baada ya kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichochunguza ripoti ya Katibu Mkuu wa umoja huo kuhusu utekelezwaji wa azimio nambari 2231 la baraza hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo alidai kuwa Marekani imeweka wazi katika kikao hicho kwamba, shughuli za makombora ya balestiki za Iran zimeondoka katika udhibiti. Pompeo alidai kuwa, Iran inakiuka azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama na ametoa wito wa kukomeshwa majaribio ya makombora ya Iran.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Dakta Muhammad Javad Zarif amejibu madai hayo ya Pompeo kwa kusema: "Suala la makombora halijawahi kuzungumziwa, na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama haliikatazi Jamhuri ya Kiislamu kufanya majaribio ya makombora."

Muhammad Javad Zarif

Makelele ya kipropaganda ya Wamarekani kuhusu miradi ya kutengeneza makombora ya Iran na ushawishi wa Jamhuri ya Kiislamu katika eneo la magharibi mwa Asia ni katika jitihada za viongozi wa White House za kutaka kuanzisha mazungumzo mapya na Tehran na kuyaweka masuala hayo mawili kwenye meza ya mjadala. Hata hivyo jitihada hizo za maafisa wa Marekani zimetajwa na maafisa wa Iran kuwa ni ndoto tupu ambayo kamwe haitatimia.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Bahram Qassemi anasema katika uwanja huo kwamba: "Matamshi yanayotolewa na maafisa wa serikali ya Marekani kuhusu ulazima wa kuwepo mazungumzo na mapatano mapya na Iran hayana thamani yoyote na Marekani ndiyo mkiukaji mkubwa zaidi wa mikataba ya kimataifa; mfano wa ukweli huo ni kukiuka kwake azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopasisha makubaliano ya nyuklia ya Iran."

Bahram Qassemi

Kufanya hadaa, kutumia mabavu na uraibu wa kuweka vikwazo ndio msingi mkuu wa sera za kigeni za serikali ya sasa ya Marekani na nchi hiyo sasa inalishikilia mateka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa shabaha ya kuzidisha uhasama wake dhidi ya Iran. Vilevile baada ya kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Marekani ilifanya kila iwezalo kuzihadaa nchi nyingine zikiwemo za Ulaya ikizitaka zifuate nyayo zake na kuharibu kabisa mapatano hayo na hatimaye kuanzishwa mazungumzo mapya. Makelele ya kipropaganda ya Mike Pompeo kuhusu makombora ya Iran ni sehemu ya sera za kihasama za Marekani dhidi ya Iran zinazokusudia kuchafua uhusiano wa nchi mbalimbali na Jamhuri ya Kiislamu. Hata hivyo Wamarekani na dunia inapaswa kutambua kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama zilvyo nchi nyingine, haitalegeza kamba hata kidogo au kufanya mapatano ya nchi yoyote nyingine kuhusu usalama na uwezo wake wa kujihami.    

Tags

Maoni