Dec 15, 2018 14:43 UTC
  • Zarif: Iran katu haitafanya mazungumzo kuhusu makombora yake

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesisitiza kwa mara nyingine kuwa, Iran haitafanya mazungumzo kuhusu makombora yake ya kujihami.

Zarif ameyasema hayo leo katika mazungumzo na mwandishi wa Televisheni ya Al Jazeera pembizoni mwa  "Mkutano wa Doha" unaofanyika katika mji mkuu wa Qatar ambapo amekanusha madai ya wakuu wa Marekani akiwemo Rais Donald Trump, kuwa eti Iran inakiuka azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Zarif amesema ni Marekani ambayo imekiuka azimio hilo na hivyo haina ustahiki wa kuituhumu Iran.

Aidha amebainisha kuwa, makombora ya Iran ni ya kujihami tu na kuzuia hujuma ya adui na kwamba bajeti ya kijeshi ya Iran ni ndogo sana ikilinganishwa na ya nchi za eneo.

Kombora la Emad lililoundwa Iran likifanyiwa majaribio

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameendelea kusema kuwa, baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya  nyuklia ya JCPOA, kimsingi ilikiuka azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama na hivyo haina ustahiki wa kuzungumza kuhusu kukiukwa azimio hilo. Nukta nyingine ambayo Zarif ameashiria ni kuwa azimio hilo haliizuii Iran kufanya majaribio ya makombora yake bali kile inachozuia ni kufanya majaribio ya makombora yanayobeba vichwa vya nyuklia. Ameongeza kuwa Iran haina nia ya kuunda silaha za nyuklia.

 

Tags

Maoni