Dec 16, 2018 15:38 UTC
  • Qassemi: Dunia imeanza mwamko na harakati ya kusitisha vita Yemen

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kumeanza kushuhudiwa mwamko na azma ya kimataifa ya kusitisha vita nchini Yemen.

Bahram Qassemi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameyasema hayo leo katika mahojiano na Shirika la Habari la Mehr na kuongeza kuwa mgogoro wa Yemen umeingia katika awamu mpya. Amesema Umoja wa Mataifa sasa unafuatilia kwa uzito hali mbaya ya kibinadamu ya watu wa Yemen na katika upande mwengine baadhi ya nchi za Ulaya zinajaribu kutumia ushawishi kuzuia muungano wa Saudia unaoongoza vita dhidi ya Yemen.

Qassemi ameashiria mpango wa mada nne wa Iran wa mwaka 2015 kuhusu kutatua mgogoro wa Yemen na kusema: "Mpango huo ni mojawapo ya njia zinazoweza kutumika kuleta utulivu na uthabiti na kwa kiasi fulani kurejesha hali ya utulivu Yemen na kuhitimisha hujuma dhidi ya nchi hiyo."

Pande hasimu Yemen zilifikia mapatano Sweden chini ya upatanishi wa Umoja wa Mataifa

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria pia matokeo ya mazungumzo ya amani ya Yemen nchini Sweden na kusema: "Katika mkutano huo wa makundi ya Wayemeni nchini Sweden chini ya upatanishi wa kimataifa kulichukuliwa hatua chanya ambazo Iran imezikaribisha."

Aidha Qassemi amesisitiza kuwa, lazima kufanyike jitihada za kutosha za Umoja wa Mataifa na nchi zote athirifu ili kusitisha hujuma ya wavamizi dhidi ya Yemen, kusitisha vita, kurejesha utulivu na kuandaa mazingira ya kuwapa misaada ya dharura watu wa nchi hiyo. Aidha ametaka mchakato wa mazungumzo ya amani ya Yemen yaliyoanza nchini Sweden uendelee.

Maoni