Jan 16, 2019 15:25 UTC
  • Jebeli: Marekani imemkamata mtangazaji wa Press TV ili kuzima sauti ya muqawama

Mkuu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, IRIB, amesema, Marekani imemkamata mtangazaji wa Televisheni ya Press TV kwa lengo la kuzima sauti ya muqawama.

Siku chache zilizopita, polisi ya Marekani ilimkamata Marzieh Hashemi, mwandishi habari mwenye asili ya Marekani ambaye ni mtangazaji katika Televisheni ya Press TV. Bi. Hashemi alikuwa ameenda Marekani kutoka Iran kutembelea familia yake na amekamatwa bila kufahamishwa sababu ya kukamatwa kwake.

Akizungumza na waandishi habari leo Jumatano, Peyman Jebeli Mkuu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Hakuna sababu yoyote ya  kukamatwa Marzieh Hashemi nchini Marekani. Kosa lake kubwa ni kuwa yeye ni mwanamke Mwislamu Mmarekani na tokea mwaka 2003 amekuwa akifanya kazi na Press TV."

Dkt. Jebeli amesema, Marekani imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali kujaribu kuzima sauti ya vyombo vya habari vya Iran na kuongeza kuwa: Mashinikizo ya Marekani kupitia kuiwekea Iran vikwazo ni jambo linaloonesha (hasira za dola hilo la kibeberu kutokana na) ustawi mzuri wa mhimili wa muqawama na huu ni ujumbe wa kimataifa kuwa mrengo wa muqawama umeushinda mrengo wa Marekani.

Mkuu wa Kitengo cha Kimataifa cha IRIB aidha ameashiria namna wakuu wa Marekani walivyomdhalilisha Marzieh Hashemi wakati akiwa korokoroni ikiwa ni pamoja na kumvua hijabu yake na kumlazimisha ale nyama ya nguruwe ambayo ni haramu kwa Waislamu na kusema, kitendo hivyo ni ukiukwaji wa wazi wa matukufu na thamani za Kiislamu. Aidha amesema mbali na kumnyima chakula cha halali, wakuu wa Marekani pia wamekataa kumpa Bi. Hashemi nguo zinazofaa katika msimu huu wa baridi kali nchini humo.

Jebeli amebainisha kuwa IRIB iko tayari kutoa msaada unaohitajika ili kuhakikisha kuwa Bi. Hashemi anaachiliwa huru. 

Wanaharakati katika mitandao ya kijamii wameanzisha kampeni maalumu za kuilazimisha Marekani kumwachilia huru Bi Marzieh Hashemi kupitia: .#FreeMarziehHashemi #Pray4MarziehHashemi.

Maoni