Feb 16, 2019 07:57 UTC
  • Kuhudhuria Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mkutano wa Munich; fursa ya kubainisha ukweli kuhusu Mashariki ya Kati

Mkutanao wa Usalama wa Munich ulianza rasmi jana Ijumaa tarehe 15 Februari kwa kuhudhuriwa na zaidi ya wakuu 35, mawaziri 50 wa mambo ya nje na mawaziri 30 wa ulinzi kutoka nchi mbali mbali duniani.

Mkutano huo utatoa fursa kwa washiriki ya kujadili na kuchunguza masuala muhimu zaidi ya kiusalama ya kieneo na ulimwengu kwa ujumla. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif, naye pia anashiriki mkutano wa usalama wa Munich, ambapo atapata fursa ya kuzungumzia siasa na sera za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na kubainisha ukweli halisi ulivyo kuhusu eneo hili la Mashariki ya Kati.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif

Mkutano wa Usalama wa Munich, uliofanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1963 na ambao umekuwa ukiendelea kila mwaka hadi hii leo, lengo lake ni kujenga hali ya kuaminiana baina ya nchi duniani pamoja na wapitishaji maamuzi ya kiusalama katika uga wa kimataifa, kwa madhumuni ya kuchangia katika kutatua kwa amani hitilafu na mapigano na kuendeleza mazungumzo ya kudumu na yasiyo rasmi ndani ya jamii ya kimataifa ya usalama.

Hata hivyo siasa za kilaghai na kizandiki za Marekani zimesababisha kuongezeka mivutano na mapigano, uungaji mkono kwa ugaidi na moto wa mizozo na uhasama baina ya mataifa ya eneo la Mashariki ya Kati, sambamba na kuenea machafuko, ukosefu wa uthabiti, umasikini, vita na misimamo ya kufurutu mpaka katika eneo hili. Siasa hizo mbovu na za miongo kadhaa sasa za Marekani zimemfanya rais wa sasa wa nchi hiyo Donald Trump atangaze na kuungama hadharani kuwa, Washington imetumia dola trilioni saba katika eneo la Mashariki ya Kati pasi na kuambulia chochote. Lakini ajabu ni kuwa, Trump mwenyewe anaendelea kufuata njia hiyo hiyo ghalati na potofu iliyoasisiwa na watangulizi wake.

Rais wa Marekani, Donald Trump

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kinyume na baadhi ya nchi za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi, haijawahi katu kupoteza mabilioni ya dola ya hazina yake kwa ajili ya kununulia silaha, kwa sababu inaamini kuwa, inao uwezo wa kukidhi mahitaji yake ya silaha na ya kiulinzi yanayokubalika katika sheria za kimataifa, kwa kutumia ujuzi wa wataalamu wa Kiirani na uwezo wake wa ndani.

Ni wazi kuwa, nguvu na uwezo wa kijeshi ilionao Iran ni mwiba wa koo kwa maadui na ngome imara ya kukabiliana na vitisho. Na ndiyo maana Marekani imekuwa ikijaribu kila mara kueneza propaganda za sumu na kutumia wenzo wa vikwazo kwa lengo la kudhoofisha uwezo wa kiulinzi wa Iran.

Kikao cha ufunguzi wa Mkutano wa Usalama wa Munich

Katika mahojiano aliyofanya jana Ijumaa na kanali ya televisheni ya NBC ya Marekani pembeni ya mkutano wa usalama wa Munich, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema: Wale wale walioafiki kuanzishwa vita dhidi ya Iraq ndio hao hao wanaotaka kuanzisha vita dhidi ya Iran, lakini watu hao, hatimaye wataelewa kuwa, kuingia vitani na Iran ni sawa na kujitia kitanzi. 

Mnamo mwezi Aprili mwaka uliopita wa 2018, wakati Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei alipohutubia hadhara ya makamanda wa Jeshi, aliashiria vitisho na njama za Marekani dhidi ya Iran na akabainisha kwamba: "Kama Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran ingekuwa ziyahofu madola makubwa na kulegeza msimamo mbele yao, leo hii pasingekuwa pamesalia athari na alama yoyote ya Iran na Uirani."

Kwa kufuata misingi yake ya kistratejia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikipigania kupatikana amani na usalama duniani. Na kwa msingi huo, Alkhamisi iliyopita kikao cha marais wa Iran, Russia na Uturuki, zikiwa nchi tatu zinazosimamia mchakato wa amani ya Syria kilifanyika mjini Sochi, Russia kikiwa na malengo ya kistratejia ya kurejesha amani na usalama nchini humo; hiyo ikiwa ni ishara ithibati tosha ya msimamo chanya wa Iran wa kupigania amani na usalama wa eneo hili.

Sayyed Baqher Zaki Oskui, mchambuzi wa masuala ya kimataifa anaizungumzia nafasi ya kieneo ya Iran kwa kusema:

"Iran imethibitisha kuwa, katika mazingira ya sasa ya eneo, inao uwezo wa kutoa mchango athirifu kwa ajili ya kuzuia vitisho vya kiusalama na kuongeza kiwango cha usalama wa kiwango fulani kwa kutumia mfumo wa kujitegemea wa kieneo wa baina ya serikali na mataifa yao. Kupambana na ugaidi, kuzuia uenezaji wa silaha za mauaji ya halaiki katika eneo, kusaidia utatuzi wa migogoro ya kikanda katika nchi za Iraq na Afghanistan na kuepusha kusambaratika na kugawanyika Syria ni masuala yanayodhihirisha mchango na nafasi ya kipekee ya Iran."

Pamoja na hayo, tajiriba inaonyesha kuwa, bila ya kufanyika jitihada za pamoja za kujenga wigo mpana wa amani na usalama, dunia itaendelea kushuhudia migogoro, machafuko na mapigano.../

Maoni