Mar 19, 2019 15:55 UTC
  • Rais wa Austria: Ulaya isikubali kufuata mdundo wa ngoma inayopigwa na Trump kuhusu Iran

Rais Alexander Van der Bellen wa Austria amelaani hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia na Iran yaliyofikiwa mwaka 2015 na vitisho alivyotoa vya kuyawekea vikwazo mashirika na makampuni yanayofanya biashara na Tehran, na kusisitiza kuwa nchi za Ulaya zisikubali kufuata mdundo wa ngoma inayopigwa na Trump.

Rais Der Bellen ameyasema hayo katika mahojiano maalumu na gazeti la Kijerumani la Die Welt. Amezihimiza nchi za Ulaya ziwe na misimamo huru katika kuchukua hatua na kutokuwa na utegemezi kwa Marekani katika sera zao kuhusiana na Iran.

Rais wa Austria ameongeza pia kuwa, mashinikizo ya Trump ya kuyataka mashirika ya Ulaya yakate uhusiano wao wa kibiashara na Iran "yamepindukia mpaka."

Rais Der Bellen amefafanua kuwa, rais wa Marekani amejitoa bila sababu yoyote kwenye makubaliano ya nyuklia ya Iran, ambayo Washington ilikuwa mratibu na mshiriki wa mazungumzo yake kwa miaka kadhaa na kisha ameyapiga marufuku makampuni ya Ulaya yasifanye biashara na Iran, huku akiyatishia kuyawekea vikwazo vikali.

Rais wa Austria ameongezea kwa kusema: "Nadhani haya sasa yanapinduka mpaka. Nchi za Ulaya zisikubali kudansi kila pale Trump anapopiga mdundo. Na hili linahusu kwenye masuala mengine pia tunayohitilafiana."

Mnamo mwezi Mei mwaka 2018, Trump alichukua uamuzi wa upande mmoja wa kujitoa Marekani kwenye makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji, maarufuku kama JCPOA na kutangaza kutekeleza kile alichokiita "vikwazo vikali kabisa" dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran licha ya upinzani wa kimataifa.

Tangu wakati huo hadi sasa, serikali ya Trump imekuwa ikijaribu kuzishinikiza nchi za Ulaya wanachama wa makubaliano ya JCPOA zifuate msimamo wa Washington na kujitoa kwenye makubaliano hayo.../

Tags

Maoni