Mar 24, 2019 15:43 UTC
  • Majeshi ya Iran yanawafikishia misaada waathirika wa mafuriko kaskazini mwa nchi

Mkuu wa Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Meja Jenerali Mohammad Baqeri amesema kuwa, vikosi vya ulinzi humu nchini vinaendesha oparesheni kamili ya kuwasaidia waathirika wa mafuruko kaskazini mwa nchi.

Hatua hiyo inafuatia amri ya  Amirijeshi Mkuu wa Majeshi yote ya Iran, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ambaye ametaka majeshi yahusike katika oparesheni za kufikisha misaada katika mikoa miwili ya Mazandaran na Golestan iliyokumbwa na mafuruko kaskazini mwa Iran.

Meja Jenerali Baqeri amewataka makamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, Jeshi la Iran,  Jeshi la Polisi na Wizara ya Ulinzi kushirkiana vilivyo katika kuimarisha zaidi jitihada za kutuma misaada ya kibinadamu, kilojistiki na kiafya katika maeneo  yaliyokumbwa na mafuruko.

Aidha Meja Jenerali Baqeri, amemteua naibu wake, Meja Jenerali, Ataollah Salehi  kuongoza timu ya makamanda wa ngazi za juu kwa lengo la kufika katika maeneo yaliyokumbwa na mafuruko  ili kusimamia oparesheni za misaada.

Waliokumbwa na mafuriko mkoani Golestan wakifikishiwa misaada ya dharura

Jana Jumamosi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambaye pia ni Amirijeshi Mkuu wa Majeshi ya Iran alitoa ujumbe kwa mnasaba wa mafuriko yaliyoikumba miji ya Golestan na Mazandaran kaskazini mwa Iran na kusisitiza kwamba kuna wajibu wa kusaidiwa watu walioathiriwa na janga hilo la kimaumbile. Aliamuru Majeshi yatume misaada mingi zaidi katika mikoa iliyoathiriwa na mafuriko.

Ayatullah Khamenei aliyasema hayo Jumamosi katika ujumbe wake huo ambapo sambamba na kuonyesha kusikitishwa kwake na hasara iliyosababishwa na mafuriko hayo amebainisha kuwa, misaada ya wananchi na kuingia vyombo vya umma katika shughuli za kutoa misaada na kufidia hasara ni jukumu muhimu ambalo linaweza kupunguza sehemu fulani ya machungu ya wananchi hao.

Kati ya misaada ya dharura inayohitajika katika eneo hilo la mafuruko ni kuwapa waathirika maeneo ya kukaa kwa muda baada ya nyumba zao kuharibiwa. Wanajeshi wa Iran hivi sasa wako mbioni kuhakikisha kuwa wananchi wote wanapata misaada wanayohitajia.

Tags

Maoni