Mar 25, 2019 14:37 UTC
  • Watu 17 wafariki dunia kwa mafuriko katika mkoa wa Fars, Iran

Kwa akali watu 17 wamefariki dunia katika mkoa wa Fars wa kusini magharibi mwa Iran na makumi ya wengine wamejeruhiwa kufuatia mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua inayoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mafuriko hayo yametokea leo katika eneo la Darvazeh Qur'an katika mji wa Shiraz ambapo kwa uchache magari 200 yamesombwa na maji huku vijiji kadhaa vikiharibiwa kabisa na kuziathiri familia nyingi.

Wengi wa wahanga wa mafuriko hayo ni wasafiri ambao walikuwa njiani kuelekea katika maeneo mbalimbali ya kitalii ikiwa ni katika muendelezo wa maadhimisho ya sikukuu ya Nairuzi ya mwaka mpya wa Hijria Shamsia.

Habari kutoka Shiraz zinasema kuwa, sehemu kubwa ya soko la Wakil mjini humo limeharibiwa huku maji yakiwa yameenea katika maeneo mengi.

Katika mkoa wa Lorestan pia ulioko magharibi mwa Iran mito imefurika maji na kusambaa katika barabara nyingi na hivyo kuleta adha na usumbufu mkubwa kutokana na kutopitika maeneo mengi ya mji huo.

Athari ya mafuriko ambayo yameyakumbwa maeneo kadhaa ya Iran

Mkuu wa Mkoa wa Lorestan ameiambia Radio Tehran kwamba, mvua na mafuriko katika mkoa huo yamesababisha hasara kubwa kwa miundombinu ya mji huo.

Wakati huo huo, mji wa Golestan wa kaskazini mashariki mwa Iran ambao nao juma lililopita ulikumbwa na mafuriko makubwa, kwa sasa asilimia 50 ya maji yaliyokuwa yameenea katika mji huo yamepungua huku misaada mbalimbali ikiendelea kupelekewa waathiriwa wa mafuriko hayo.

Katika upande mwingine, Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa la Iran limetahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea mafuriko katika mikoa 12 hapa nchini katika kipindi cha siku tatu zijazo.

Tags

Maoni