Apr 22, 2019 17:27 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Uhusiano wa Iran na Pakistan lazima ustawishwe hata kama maadui watachukia

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, uhusiano wa mataifa mawili ya Iran na Pakistan ni wa moyoni uliokita mizizi vyema na kusisitiza kuwa, inabidi uhusiano huo uimarishwe kadiri inavyowezekana hata kama maadui wa mataifa haya mawili watachukia.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo jioni alipoonana na Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, masuala ya usalama wa mipakani wa nchi hizo mbili ni muhimu sana.

Ameongeza kuwa, magenge ya kigaidi yanayovuruga usalama katika mipaka ya nchi hizi mbili yanadhaminiwa kifedha na kisiasa  na maadui na kwamba moja ya malengo yao ya kuchafua usalama katika mipaka ya Iran na Pakistan ni kutaka kuzigombanisha nchi hizi mbili. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia uhusiano mkongwe na wa kihistoria wa mataifa mawili ya Iran na Pakistan na kuongeza kuwa, ustawi mkubwa na heshima ya Bara Hindi ilikuwepo katika zama ambazo Waislamu walikuwa wakitawala eneo hilo na pigo kubwa lililotolewa na wakoloni wa Kiingereza dhidi ya watu wa eneo hilo ni kitendo chake cha kuangamiza ustaarabu mtukufu wa Kiislamu wa Bara Hindi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alipotembelewa na Waziri Mkuu wa Pakistan, Imran Khan. (Tehran Aprili 22, 2019).

 

Vile vile ameishukuru serikali ya Pakistan kwa misaada yake kwa wahanga wa mafuriko ya hivi karibuni ya nchini Iran na kuongeza kuwa, hatua ya Waziri Mkuu Imran Khan ya kuanzia Mash'had safari yake ya kuitembelea Iran ambako alikwenda kufanya ziara katika Haram toharifu ya Imam Ali bin Musa al Ridha AS ni ishara nzuri na kwamba Iran ina matumaini kwa baraka za Imam Ridha AS safari ya Waziri Mkuu huyo wa Pakistan hapa Iran itakuwa na faida kubwa kwa nchi zote mbili.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Pakistan amesema katika mazungumzo hayo kwamba kuna watu hawataki kuona uhusiano wa Tehran na Islamabad unastawi lakini amesema: Tutaendelea kufanya juhudi za kuimarisha zaidi na zaidi uhusiano huo.

Vile vile amesema, wizi na uporaji mkubwa zaidi ya mali za Bara Hindi ulifanywa katika enzi za ukoloni wa Uingereza. Ameongeza kuwa Waingereza wamepora utajiri wote wa India, wameangamiza mfumo wake wa masomo na walikuwa wanaitaja India kuwa ni koloni lao la vito vya thamani.

Maoni