Apr 23, 2019 13:34 UTC
  • Sisitizo la Kiongozi Muadhamu la Kuimarishwa uhusiano wa Iran na Pakistan

Safari ya Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan humu nchini na maafikiano muhimu yaliyofikiwa kati ya jumbe za ngazi za juu za nchi mbili yamefungua ukurusa mpya wa ushirikiano kati ya Tehran na Islamabad.

Moja ya nukta muhimu za safari hiyo ni kukutana Waziri Mkuu wa Pakistan na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ambapo Kiongozi Muadhamu alisisitiza umuhimu wa kulindwa uhusiano mzuri kati ya nchi mbili hizi muhimu za Kiislamu. Alipomkaribisha ofisini kwake Waziri Mku huyo wa Pakistan pamoja na ujumbe alioadamana nao, Ayatullah Khamenei huku akisema kwamba uhusiano uliopo kati ya mataifa ya Iran na Pakistan ni wa dhati na wa kina, alisisitiza kwamba uhusiano wa nchi mbili unapaswa kuimarishwa zaidi licha ya kuwepo uhasama wa maadui. Kwa upande wake Imran Khan amesema katika mazungumzo hayo kwamba licha ya kuwa baadhi ya watu hawataki kuona uhusiano wa nchi yake na Iran ukiimarika ameongeza kwamba: 'Tutafanya juhudi za kuboresha uhusiano wa nchi mbili na kufanya mawasiliano ya mara kwa mara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.'

Matamshi na uamuzi wa kistratijia wa Tehran na Islamabad wa kupambana na ugaidi katika mipaka yao ya pamoja, auamuzi ambao pia umependekeza kubuniwa kwa kikosi cha pamoja cha radiamali ya haraka, unabainisha wazi utambuzi wa pande mbili juu ya maslahi ya mataifa mawili na umuhimu wa kuchukuliwa hatua za pamoja kwa lengo la kupambana na vitishio vya pamoja. Kama alivyosisitiza Kiongozi Muadhamu, huku akiashiria vyanzo vya kihistoria vya uhusiano wa nchi mbili, moja ya malengo ya harakati zilizo dhidi ya usalama katika mipaka ya Iran na Pakistan ni kuchafua uhusiano wa nchi hizi.

Imran Khan (kushoto) akizungumza na Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kwa mtazamo huo maafikiano ya Iran na Pakistan katika uwanja wa ushirikiano wa kiusalama na kubuniwa kikosi cha radiamali ya haraka kwa ajili ya kupambana na ugaidi ni jibu tosha kwa harakati hizo. Ugaidi kwa vyovyote vile una madhara iwe ni katika eneo au katika mipka ya nchi mbili. Iran na Pakistan zina uzoefu mchungu kutokana na makundi ya kigaidi. Kukaririwa vitendo vya ugaidi kunathibitisha wazi kwamba uingiliaji wa askari wa kigeni kwa kisingizio cha kuleta amani na kupambana na ugaidi, kama inavyoshuhudiwa nchini Afghanistan tokea kuvamiwa nchi hiyo na Marekani na kutumwa nchini humo askari wa Nato, hauna manufaa yoyote kwa mataifa ya eneo. Kinyume na inavyodaiwa, uingiliaji huo wa kijeshi umepelekea kuongezeka kwa makundi ya kigaidi na uzalishaji wa madawa ya kulevya nchini humo jambo linalotishia usalama wa eneo zima. Kwa matazamo wa wajuzi wa mambo, ukosoaji wa Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan kwa siasa za kijuba za Marekani na msimamo wa kiuadui wa Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Islamabad, inaweza kuchukuliwa kuwa ni fursa nzuri kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa nchi hiyo na jirani yake Iran, na hasa kuhusiana na masuala ya kudhaminiwa usalama katika mipaka ya pamoja, jambo ambalo pia linapewa umuhimu mkubwa na Pakistan.

Jumbe za ngazi za juu za Iran na Pakistan zikifanya mazungumzo mjini Tehran

Kuhusiana na suala hilo, Imran Khan amesema: 'Tokea mwanzo nimekuwa nikipinga uingiliaji na uwepo wa kijeshi wa Marekani katika nchi za Afghanistan na Iraq na leo pia ninapinga vikali kukaliwa kwa mabavu milima ya Golan ya Syria pamoja na kutangazwa mji mtakatifu wa Quds kuwa eti ni mji mkuu wa Israel na vilevile Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Tunalichukulia jambo hilo kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Hivyo tunaweza kusema kwamba hivi sasa uhusiano wa Iran na Pakistan uko kwenye njia sahihi. Nchi hizi zikiwa nchi jirani, zimeamua kuchukua hatua muhimu ya kuimarisha ushirikiano wao wa kistratijia na kiusalama kwa kubuni kikosi cha pamoja kwa ajili ya kupambana na ugaidi. Bila shaka ushirikiano huo utakuwa na athari kubwa katika uhusiano wa baadaye wa nchi hizi na pia unaweza kuchukuliwa kuwa mfano mzuri wa kuigwa na majirani wegine wa eneo kwa ajili ya kuboresha uhisano wao. Kutembea kwenye njia hii pia kunaweza kuimarisha ushirikiano katika nyanja nyingine za uchumi na hasa za kudhamini nishati ambayo inahitajika sana na Pakistan.

 

Maoni