Apr 23, 2019 14:10 UTC
  • IRGC: Ikibidi, Iran itafunga lango bahari la Hormuz

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) limesema lango bahari la Hormuz ni njia ya kimataifa ya majini na kwamba Iran haitakuwa na chaguo jingine ghairi ya kulifunga lango hilo la kistratajia iwapo itazuiwa kulitumia.

Kamanda wa Kikosi cha Majini cha IRGC, Admeri Alireza Tangsiri amesema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya Al-Alam, ikiwa ni radimali kwa tangazo la Rais Donald Trump, ambaye jana alisema kuwa Marekani haitarefusha kibali cha kununua mafuta ya Iran, kwa nchi ambazo zilikuwa zimeruhusiwa kuyanunua licha ya vikwazo vya Washington. 

Amebainisha kuwa, "Iwapo kutaibuka vitisho vyovyote, hatutasita kulinda maji yetu. Tutalinda heshima na hadhi yetu, na tutatoa jibu mwafaka kwa lengo la kulinda na kutetea haki za taifa la Iran."

Mwezi Novemba mwaka jana, Marekani ilianza kutekeleza vikwazo vya kibenki dhidi ya sekta ya mafuta ya Iran, lakini ikazipa kibali cha kuendelea kununua mafuta ya nchi hii wanunuzi wakubwa wa bidhaa hiyo kutoka Iran ambazo ni China, India, Japan, Korea Kusini, Taiwan, Uturuki, Italia na Ugiriki, lakini Trump ametangaza kuwa atakibatilisha kibali hicho kuanzia mwezi ujao wa Mei.  

Ramani inayoonesha lango bahari la Hormuz

Wataalamu wa masuala ya mafuta wa Iraq wameonya kuwa, endapo lango bahari la Hormuz litafungwa, bei ya pipa moja la mafuta itafika dola 400, kutoka bei ya dola 50 hadi 70 ya sasa.

Mwaka uliopita, na katika jibu alilotoa kwa vitisho vya Marekani kwamba itahakikisha mafuta ya Iran yanasusiwa, Rais Hassan Rouhani aliwahutubu na kuwaeleza kinagaubaga viongozi wa serikali ya Washington kwamba Jamhuri ya Kiislamu ina machaguo mengi ya kutumia kwa ajili ya kukabiliana na vitisho vya Marekani, mojawapo likiwa ni kulifunga lango bahari la Hormuz.

Tags

Maoni