Apr 26, 2019 04:48 UTC
  • Iran yalitaka jeshi la Sudan kukabidhi madaraka kwa amani bila ya uingiliaji wa kigeni

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelitaka jeshi la Sudan kukabidhi madaraka kwa amani kwa raia bila ya uingiliaji wa madola ya kigeni.

Sayyid Abbas Mousavi amesema hayo mjini Tehran na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafuatilia kwa karibu matukio ya Sudan na maandamano ya wananchi wa nchi hiyo na inaamini kwamba kuna wajibu wa kusikilizwa matakwa ya haki ya wananchi hao ikiwa ni pamoja na kukabidhiwa madaraka kwa utawala wa kiraia kwa njia za maani, kutotumia nguvu na mabavu na kutoruhusu madola ya kigeni kuingilia masuala ya ndani ya Sudan.

Amesisitiza kuwa, kukabidhiwa haraka madaraka kwa raia na kurekebishwa maamuzi yasiyo sahihi yaliyochukuliwa na utawala uliopita kama uamuzi wa kutuma wanajeshi wa Sudan kwenda kuua ndugu zao wasio na hatia huko Yemen ni miongoni mwa mambo ambayo yanaweza kutoa mchango mkubwa wa kutatuliwa matatizo yaliyopo na kufanikishwa malengo ya taifa kubwa la Sudan.

Maandamano ya wananchi nchini Sudan

 

Maandamano ya wananchi yanaendelea nchini Sudan baada ya jeshi kujaribu kuzima maandamano hayo kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyomng'oa madarakani Rais Omar Hassan al Bashir. Hasira za wananchi wa Sudan ziliongezeka baada ya wanajeshi hao kuunda baraza la kijeshi na kutangaza kuwa litatawala nchi hiyo kwa muda wa miaka miwili.

Maandamano hayo ya wananchi yameongeza mashinikizo kwa wanajeshi hao kiasi kwamba, juzi Jumatano, Walitangaza kujiuzulu muda mfupi baada ya mazungumzo kati ya wanajeshi hao na viongozi wa maandamano ya wananchi huko Sudan.

Maoni