Feb 12, 2016 08:08 UTC
  • Russia: Kutuma vikosi vamizi Syria kutachochea Vita vya Dunia

Waziri Mkuu wa Russia ametahadharisha juu ya kutumwa vikosi vya kigeni nchini Syria na kusema kuwa hatua hiyo haitakuwa na tija nyingine ghairi ya kuchochea "Vita Vipya vya Dunia".

Dmitry Medvedev ameyasema hayo katika mahojiano na Gazeti la Ujerumani la Handelsblatt na kuongeza kuwa, kuna haja ya kutoa fursa ya kufanyika mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Syria badala ya kupanga kutuma askari vamizi nchini humo. Medveded ameitaka Marekani na Saudia kutathmini kwa makini suala la kutuma vikosi Syria akisisitiza kwamba, hatua hiyo itachochea vita visivyo na mwisho duniani. Kauli hii inakuja siku chache baada ya Saudi Arabia kusema kuwa iko tayari kutuma askari wake nchini Syria iwapo itapata ridhaa ya Marekani. Hii ni katika hali ambayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Walid al-Muallem amesema kuwa shambulio lolote la ardhini litakalofanywa ndani ya ardhi ya Syria bila ya idhini ya serikali ya nchi hiyo litahesabiwa kuwa ni uvamizi; na wale watakaoivamia Syria watarudi makwao wakiwa kwenye majeneza. Mbali na Saudia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Utawala wa Aal-Khalifa wa Bahrain umesema uko tayari kutuma askari wake wa nchi kavu nchini Syria, eti kupambana na wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, hatua ambayo Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (SEPAH) limesema ni kichekesho na utani wa kisiasa.

Tags

Maoni