Aug 28, 2016 07:41 UTC
  • Wapalestina wasisitiza kupandishwa kizimbani wazayuni waliotenda jinai

Wapalestina wameendelea kutoa wito wa kutaka wazayuni waliotenda jinai katika vita vya siku 50 dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza wapandishwe kizimbani kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Baada ya kupita miaka miwili tangu vita vya siku 50 vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina wa Ukanda wa Gaza vilivyosababisha kuuawa Wapalestina zaidi ya 2,000 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo, Wapalestina wangali wanasisitiza haki na uadilifu utendeke kwa ajili ya watu waliouliwa bila ya hatia katika vita hivyo.

Watoto wengi Wapalestina waliuliwa katika jinai za siku 50 zilizofanywa na Israel Gaza

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai imeanza kufanya uchunguzi wa awali kuhusu jinai zilizofanywa na Israel katika vita vya siku 50 vya mwaka 2014.

Baada ya jeshi la utawala wa Kizayuni kutangaza kuwa mafaili saba yanayohusiana na mauaji ya raia wa Palestina yameshafungwa, Wapalestina wameihimiza mahakama ya ICC iharakishe uchunguzi wake juu ya suala hilo.

Mustafa Barghuthi, Katibu wa Harakati ya Ubunifu wa Kitaifa ya Palestina amesema Mahakama ya Kimataifa ya Jinai imekuwa ikisuasua katika kuchukua uamuzi wa kuanzisha uchunguzi kuhusu vita vya Gaza.

Mustafa Barghuthi, Katibu wa Harakati ya Ubunifu wa Kitaifa ya Palestina

Barghuthi amesisitiza kuwa kuna ulazima wa kufanyika uchunguzi wa suala hilo na kuongeza kwamba haipasi kuiruhusu Israel ijivue na mas-ulia na dhima ya jinai ilizotenda katika vita vya siku 50 dhidi ya Gaza.

Zaidi ya Wapalestina 2,300 waliuawa shahidi na maelfu ya wengine walijeruhiwa katika mashambulio ya siku 50 mtawalia yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni mwaka 2014 dhidi ya Ukanda wa Gaza.../

 

 

Tags

Maoni