Nov 30, 2016 15:04 UTC
  • Hashdu Shaabi yakomboa vijiji 2, yaokoa familia elfu 2 Mosul, Iraq

Kikosi cha kujitolewa cha Hashdu Shaabi kinachoshirikiana na jeshi la Iraq katika operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi na la wakufurishaji la Daesh kimefanikiwa kukomboa vijiji viwili vya mji huo sambamba na kuokoa familia zaidi ya elfu mbili zilizokuwa zikiishi kwenye mazingira magumu sana katika vijiji hivyo.

Shirika la habari la Kiarabu la al-Furat limeripoti kuwa, mapema leo Jumatano wanamapambano wa Hashdu Shaabi wamefanikiwa kukomboa vijiji vya al-Buthah na al-Salehiyah vilivyoko kusini magharibi mwa Mosul, yapata kilomita 400 kaskazini mwa mji mkuu Baghdad. Aidha familia 2,300 zilizokuwa zinatumiwa na matakfiri wa Daesh kama ngao katika hujuma zao za kigaidi wameokolewa kwenye operesheni hiyo.

Wakati huo huo, Luteni Jenerali Raed Shaker Jawdat, Kamanda wa Vikosi vya Polisi ya Federali amesema askari wa Iraq wamewaangamiza wanachama tisa wa Daesh katika operesheni nyingine iliyofanyika leo kwenye kijiji cha Um al-Masaed.

Miongoni mwa familia zilizokolea na Hashdu Shaabi, Mosul, Iraq

Aidha duru za habari zimearifu kuwa, kwenye operesheni nyingine tofauti katika mji wa Hamam al-Alil, yapata kilomita 30 kusini mwa Mosul, wanajeshi wa Iraq wakishirikiana na wanamapambano wa kujitolea wa Hashdu Shaabi wamegundua handaki la silaha za Daesh na kupata fulana sita zinazotumiwa na walipuaji wa kujitolea muhanga pamoja na maroketi kadhaa.

Operesheni ya kukomboa Mosul ambayo ni makao makuu ya mkoa wa Nainawa (Nineve) nchini Iraq ilianza tarehe 17 mwezi uliopita wa Oktoba na magaidi wa Daesh wanaendelea kufurushwa kutoka maeneo mengi ya mji huo.

Mji huo ambao ulikaliwa kwa mabavu na kundi la kigaidi la Daesh mwaka 2014, umeshuhudia mauaji makubwa ya maelfu ya vijana ambao walikataa kushirikiana na genge hilo la wakufurishaji la Kiwahabi. 

Tags

Maoni