Dec 17, 2016 04:24 UTC
  • Sheikh Sabri: Kuuhamishia ubalozi wa Marekani Quds ni kutangaza vita na Wapalestina

Khatibu wa Sala ya Ijumaa katika msikiti mtukufu wa Al-Aqsa, Palestina inayokaliwa kwa mabavu amesema, kuhamishiwa Baitul Muqaddas ubalozi wa Marekani ulioko Tel Aviv na kuitambua rasmi Quds kuwa mji mkuu wa utawala bandia wa Israel ni sawa na kutangaza vita na Wapalestina.

Sheikh Ikrima Sabri amesema, ahadi aliyotoa rais mteule wa Marekani Donald Trump ya kuuhamishia Quds ubalozi wa nchi hiyo ulioko Tel Aviv ni dhulma kwa Wapalestina kwa sababu hatua hiyo na kuitambua Baitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa Israel ina maana ya kutozitambua haki za Wapalestina.

Khatibu wa Sala ya Ijumaa wa msikiti wa Al-Aqsa amefafanua kwamba, ikiwa ahadi hiyo ya Trump itatimizwa, na Quds ikawa mji mkuu wa Israel, hiyo itakuwa sawa na kutangaza vipya, si kwa Wapalestina pekee bali kwa Ulimwengu wa Waarabu na wa Kiislamu pia.

Sheikh Sabri amesisitiza kuwa harakati mpya zinazofanywa na Israel na Marekani dhidi ya Quds Tukufu zinakinzana na maazimio ya Umoja wa Mataifa yanayoeleza bayana kuwa Baitul Muqaddas ni mji unaokaliwa kwa mabavu.

Mandhari ya mji mtukufu wa Baitul Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu

Nir Barkat, Meya wa mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni ametangaza kuwa, kwa kuendelezwa ujenzi wa ubalozi mdogo wa Marekani huko Quds, jengo hilo litatumika kama ubalozi mdogo na pia ubalozi rasmi wa Marekani katika mji huo.

Hapo kabla pia Kellyanne Conway, mshauri wa rais mteule wa Marekani alitangaza kuwa kuuondoa ubalozi wa nchi hiyo ulioko Tel Aviv na kuuhamishia Baitul Muqaddas ni miongoni mwa vipaumbele vya Trump.../

Tags

Maoni