• Ibrahim al Jaafari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq
    Ibrahim al Jaafari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amesema kuwa nchi yake haiwezi kuiruhusu Marekani kuweka kambi zake za kijeshi katika ardhi ya nchi hiyo.

Ibrahim al Jaafari amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la al Sharq al Awsat linalochapishwa mjini London Uingereza na kuongeza kuwa, ilichokubali Iraq ni kuweko washauri wa kijeshi tu wa Marekani nchini humo kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa nchi hiyo. Amesema nchi mbili za Iraq na Marekani zimekubaliana tu kushirikiana katika utekelezaji wa makubaliano ya kiistratijia na si kuwekwa kambi za kijeshi za Marekani nchini humo.

Kabla ya hapo, Waziri Mkuu wa Iraq, Haydar al Abadi alisisitiza kuwa, genge la kigaidi la Daesh (ISIS) limekaribia kuangamizwa kikamilifu nchini humo, hivyo, wakati umefika wa kupunguzwa idadi ya askari wa kigeni wakiwemo wa Marekani waliotumwa nchini Iraq kuisaidia serikali kukabiliana na magaidi.

Wanajeshi wa Marekani nchini Iraq

 

Mwaka 2011 Marekani ilitangaza kuondoa wanajeshi wake nchini Iraq. Hata hivyo mwaka 2014 baada ya kuundwa genge la Daesh, Marekani ilituma tena wanajeshi wake huko Iraq kiasi kwamba hivi sasa kuna karibu wanajeshi elfu tano wa Marekani nchini humo.

Katika sehemu nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq ameelezea matumaini yake ya kuzidi kukurubiana nchi za Kiarabu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hususan baada ya Tehran kuiandikia barua Kuwait na kusisitizia wajibu wa kujiepusha na machafuko nchi zinazopakana na Ghuba ya Uajemi.

Tags

Mar 29, 2017 13:54 UTC
Maoni