Apr 12, 2017 03:52 UTC
  • Brigedia Jenerali Rasool: Daesh inadhibiti chini ya 7% ya ardhi ya Iraq

Jeshi la Iraq limesema idadi ya ngome zilizokuwa zikidhibitiwa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh nchini humo imedidimia kutoka asilimia 40 hadi chini ya asilimia 7 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Msemaji wa Jeshi la Iraq, Brigedia Jenerali Yahya Rasool aliwaambia waandishi wa habari mjini Baghdad hapo jana kuwa, Daesh ilikua inadhibiti asilimia 40 ya ardhi ya Iraq mwaka 2014, lakini kufikia Machi 31 mwaka huu, genge hilo la kigaidi lilikuwa linashikilia asilimia 6.8 tu ya ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu kwa sasa.

Katika muda wa miaka miwili iliyopita, Daesh au ISIS imekuwa ikipoteza udhibiti wa ngome zake nyingi na sasa kundi hilo limejaribu kushadidisha mashambulizi yake ya kulipiza kisasi bila mafanikio, hususan katika mji wa kaskazini mwa Iraq wa Mosul. 

Vifaru vya Jeshi la Iraq mjini Mosul

Mapema mwezi huu, jeshi la Iraq lilitangaza habari ya kuuliwa kinara nambari mbili wa kundi la Daesh katika shambulizi la anga, magharibi mwa mkoa wa al-Anbar nchini humo, kwa jina Ayad Hamid Khalaf Al-Jumaili, maarufu kwa jina la Abu Yahya.

Hivi karibuni Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi alisema kuwa ushindi dhidi ya kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh unakaribia huku akisisitizia umuhimu wa wananchi na jamii ya kimataifa kuendelea kuiunga mkono Iraq katika mapambano yake dhidi ya ugaidi.

Tags

Maoni