• Kushindwa vikosi vamizi vya Saudia huko Yemen na wasiwasi wa Marekani

Waziri wa Ulinzi wa Marekani amesema akiwa nchini Saudi Arabia kwamba, kuna ulazima wa kuchukuliwa hatua za kuzuia mashambulio ya makombora ya jeshi na vikosi vya wananchi wa Yemen dhidi ya ngome za Saudia.

Jenerali James Mattis akiwa katika safari yake ya kulitembelea eneo la Mashariki ya Kati, siku ya Jumanne aliwasili nchini Saudia na akabadilishana mawazo na viongozi wa Riyadh kuhusiana na kusimamishwa mashambulio ya makombora ya kikosi cha Harakati ya Ansarullah ya Yemen  dhidi ya Saudia.

Misimamo ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani inabainisha kwamba, Washington ina lengo la kuficha ukweli wa mambo huko Yemen. Katika uwanja huo, Marekani ikitumia propaganda inataka kupotosha ukweli wa mambo kuhusiana na mashambulio ya makombora ya Harakati ya Ansarullah ambayo kimsingi ni jibu la uvamizi wa Saudia dhidi ya ardhi ya Yemen.

Jenerali James Mattis, Waziri wa Ulinzi wa Marekani

Aidha msimamo huo wa Waziri wa Ulinzi wa Marekani unabainisha wasiwasi na hofu inayoongezeka kuhusiana na uwezo wa muqawama wa wananchi wa Yemen ambao kivitendo umevuruga kabisa mahesabu ya vikosi vamizi vya Saudia na waungaji mkono wake.

Vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Yemen vikitegemea uwezo wao wa ndani na kutengeneza makombora mbalimbali vimekuwa vikitoa majibu kwa jinai za Saudia kwa kushambulia kambi za kijeshi za Saudia katika maeneo mbalimbali ya Yemen na wakati mwingine kurusha makombora hayo hata jirani kabisa na mji mkuu Riyadh.  

Kushindwa vikosi vamizi vya Saudia katika kufikia malengo yake ya kivamizi pamoja na waungaji mkono wake katika vita vya niaba dhidi ya Yemen kumewatia wasiwasi mkubwa waungaji mkono wake. Hatua hiyo imewafanya viongozi wa Marekani katika siku za hivi karibuni kutoa matamshi ya wazi zaidi na yaliyojaa chuki dhidi ya wananchi wa Yemen.

Jambo hilo linaonyesha kuwa, nyuma ya pazia katika vita vya niaba vya Saudia dhidi ya Yemen kuna malengo ya wafanya njama katika kiwango cha hali ya juu. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana Marekani inaona kuwa, kushindwa Saudia katika vita huko Yemen kutakuwa pigo kubwa kwake.

Wanajeshi wa Saudia wamekuwa wakiuawa huko Yemen

Hali hiyo ndiyo imeifanya Marekani kuwa na lengo la kuokoa jahazi la Saudi linalozama huko Yemen kwa kuingia yenyewe katika uwanja wa kusukuma mbele siasa zake ili kuzuia kushindwa zaidi kibaraka wake katika Mashariki ya Kati yaani Saudi Arabia.

Katika uwanja huo, kikosi maalumu cha Marekani kimefanya operesheni kadhaa za kijeshi katika mikoa ya Baydha, Abin na Hadhramaut huko Yemen. Hata hivyo lililo wazi mbele ya fikra za waliowengi ulimwenguni na katika nchi za Kiarabu ni kwamba, harakati hizo ni uungaji mkono wa moja kwa moja na msaada wa kilojistiki wa Marekani kwa Saudia katika uvamizi wake dhidi ya Yemen.

Kuna ripoti zinazoonyesha kuwa, Marekani, Uingereza, Saudia na Imarati zimefikia makubaliano ya kuidhibiti pwani ya magharibi mwa Yemen. Lengo la makubaliano hayo ni kulidhibiti Lango Bahari la Bab al-Mandab ambalo ni eneo muhimu na la kiistratejia na hivyo kuviwezesha vikosi vya muungano vamizi kuudhibiti mji wa bandari wa Al Hudaydah.

Katika mazingira hayo, weledi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa, mipango hiyo inalenga kuigawanya nchi hiyo katika sehemu kadhaa ndogo ndogo na hivyo kuidhoofisha na hatimaye kuisambaratisha kabisa.  

 

 

 

Apr 20, 2017 02:25 UTC
Maoni