• Radiamali ya Wapalestina kwa njama za Mamlaka ya Ndani ya Palestina dhidi ya muqawama

Maamuzi ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina yaliyo dhidi ya muqawama na mapambano ya wananchi wa Palestina yangali yanaendelea kushuhudiwa.

Katika uwanja huo, Mamlaka ya Ndani ya Palestina imeliweka katika mipango yake suala la kupokonywa silaha makundi ya muqawama wa Palestina hatua ambayo imekabiliwa na radiamali kali kutoka kwa Wapalestina. Dakta Mahmoud al-Zahar, mjumbe wa Idara ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisitiza kuwa,  hakuna mtu yeyote huko Palestina anayekubaliana na takwa la Mamlaka ya Ndani ya Palestina la kupokonywa silaha Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS. Dakta al-Zahar sambamba na kuashiria katika taarifa yake hatua ya hivi karibuni ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina ya kukata umeme na kupunguza mishahara ya wafanyakazi huko Gaza ametangaza kuwa, kusimama kidete wananchi wa Gaza kutapelekea njama na mipango ya Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kutokuwa na natija nyingine bighairi ya kushindwa na kugonga mwamba.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Mahmoud Abbas amechukua hatua hiyo wakati huu wa kukaribia kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Donald Trump wa Marekani akiwa na nia ya kuishinikiza Hamas na kuifanya isalimu amri mbele ya matakwa yake hususan kuhusiana na kadhia ya upokonywaji silaha harakati ya Hamas. Kukatwa umeme katika eneo la Ukanda wa Gaza na kupunguzwa mishahara ya wafanyakazi kumelifanya eneo hilo likabiliwe na hali mbaya mno.

Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina

Sisitizo la Mamlaka ya Ndani ya Palestina la kupokonywa silaha muqawama wa wananchi linakwenda sambamba na kushadidishwa vitisho vya viongozi wa utawala haramu wa Israel vya kutaka kuikalia kwa mabavu Gaza, jambo linaloonyesha kuweko uratibu maalumu baina ya pande mbili hizo.

Katika uwanja huo, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel amesisitiza bayana kwamba, chaguo la kuikalia kwa mabavu Gaza lingali katika mipango ya utawala huo.

Hapana shaka kuwa, kuwa pamoja Mamlaka ya Ndani ya Palestina na Israel na kufuata siasa za kupenda kujitanua na za kivamizi za Wazayuni kunahesabiwa kuwa ni usaliti wa wazi kwa malengo matukufu ya Palestina.

Ni jambo lisilo na shaka kwamba, kupokonywa silaha muqawama tena katika kipindi ambacho adui anapiga ngoma ya vita na anasubiri fursa tu ili ayakalie kwa mabavu maeneo zaidi ya ardhi za Palestina hakuna maana nyingine bighairi ya kusalimu amri Wapalestina mbele ya Wazayuni maghasibu. Siku zote makundi ya mapambano ya Palestina yamekuwa yakikosoa vikali ushirikiano wa kiusalama baina ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na utawala ghasibu wa Israel. Ushirikiano huo wa kiusalama unatajwa kuwa kizingiti kikuu cha operesheni dhidi ya Wazayuni.

Inaelezwa kuwa, katika magereza ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina kuna wanaharakati wengi wa Kipalestina ambao walitiwa mbaroni na maafisa wa usalama wa mamlaka hiyo baada ya kutekeleza operesheni za kijeshi dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Tukichunguza utendaji wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ambayo iliasisiwa baada ya mwenendo wa mapatano katika Mashariki ya Kati na kutiwa saini mkataba wa Oslo inawezekana kufahamu kwamba, harakati za mamlaka hiyo zimekuwa na lengo la kusukuma mbele gurudumu la siasa za kupenda kujitanua na za kuzusha mifarakano za Israel katika ardhi ya Palestina. 

Wanamapambano wa Hamas

Kuendelea hatua za Mamlaka ya Ndani ya Palestina za kuwatia mbaroni wanaharakti wa Kipalestina na kusisitiza kupokonywa silaha muqawama wa Palestina na wakati huo huo kuwa kwake na nafasi haribifu katika siasa za Palestina, kivitendo kumekuwa kikwazo kikuu cha kupatikana umoja na mshikamano baina ya Wapalestina. Hapana shaka kuwa, siasa hizo za Mamalaka ya Ndani ya Palestina zitazidi kuifanya iendelee kuchukiwa  na wananchi wa Palestina.

Linalofahamika wazi ni kuwa, baada ya wananchi wa Palestina kuona mafanikio ya muqawama ambao katika miaka ya hivi karibuni umetoa pigo kubwa kwa Israel katika nyanja mbalimbali za kisiasa na kijeshi, wamefikia natija hii kwamba, njia pekee ya kufikia malengo yao matukufu ni kudumisha mapambano dhidi ya utawala haramu wa Israel.

Apr 21, 2017 02:34 UTC
Maoni