Apr 21, 2017 06:28 UTC
  • Mafanikio ya jeshi la Syria licha ya mashambulizi ya kiadui ya Marekani

Licha ya Marekani kufanya shambulizi la makombora dhidi ya kambi ya kijeshi ya Shayrat ya jeshi la Syria hatua ambayo inaonesha wazi uungaji mkono wa Marekani kwa magenge ya kigaidi yanayofanya jinai nchini humo, lakini jeshi la Syria linazidi kupata mafanikio katika mapambano yake dhidi ya magaidi wakufurishaji kwenye mikoa na maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Hivi sasa vikosi vya ulinzi vya Syria kwa kushirikiana na vikosi vya muqawama vimeanzisha operesheni ya kukomboa mji mkubwa na muhimu wa Halfaya wa kaskazini mwa mkoa wa Hama, magharibi mwa Syria. Operesheni hiyo imeanza baada ya jeshi la Syria na vikosi vya muqawama kukomboa vitongoji vingine muhimu magharibi mwa nchi hiyo kutoka mikononi mwa magenge ya kigaidi. Jeshi la Syria linaendelea kushambulia pia maeneo mengine ya magaidi kwa kutumia mizinga na makombora, suala ambalo linazidi kuthibitisha kuwa shambulio la makombora la Marekani dhidi ya jeshi la Syria halikuathiri nguvu za jeshi hilo.

Mafanikio hayo yamepatikana huku jeshi la Syria na waitifaki wake wakizidi kupata ushindi na kukomboa maeneo zaidi ya karibu Halab (Aleppo). Mwezi Disemba mwaka jana, jeshi la Syria lilifanikiwa kukomboa eneo la mashariki mwa Halab, na huo ulihesabiwa ni ushindi mkubwa sana kwa jeshi hilo na vikosi vya muqawama. Magenge ya kigaidi na waungaji mkono wao kama vile Marekani, Uturuki, Saudi Arabia na Qatar hawakutarajia kabisa kwamba jeshi la Syria lingeliweza kukomboa mji huo muhimu sana. 

Kituo cha kijeshi cha Shayrat cha Syria kilichoshambuliwa na Marekani

 

Tarehe 7 Aprili mwaka huu, Marekani ilifanya shambulio la makombora dhidi ya kituo cha jeshi la anga la Syria huko Shayrat kwa madai kuwa Syria imetumia silaha za kemikali katika vita vyake dhidi ya magaidi. Shambulio hilo la Marekani lilifanyika hata kabla ya kufanyika uchunguzi kuhusu madai ya kutumika silaha hizo, na je, ni kweli silaha hizo zilitumika na kama zilitumika, je, ni serikali ya Syria iliyofanya mashambulizi hayo au la. Marekani haikusubiri uchunguzi wowote ule na hadi hivi sasa waungaji mkono wa magenge ya kigaidi wanaendelea kukwamisha juhudi za nchi kama Iran na Russia za kutaka uchunguzi ufanyike wa kubaini ukweli wa madai hayo.

Wachambzi wa mambo wanaamini kuwa, Marekani ilifanya shambulio la makombora dhidi ya wanajeshi wa Syria huko Homs, baada ya kuona magaidi wamelemewa vibaya. Kwa mtazamo wa wachambuzi hao, lengo la Marekani lilikuwa ni kurudisha mori wa kupigana wa magaidi waliokata tamaa kikamilifu nchini Syria.

Amma mkoa wa Hama nao una umuhimu mkubwa na ndio maana jeshi la Syria na waitifaki wake wameelekeza nguvu zao kwenye ukombozi wa mkoa huo ambao unapakana na mkoa wa Idlib ambao nao una umuhimu mkubwa. Sehemu kubwa ya mkoa wa Idlib bado iko mikononi mwa magenge ya kigaidi.

Wananchi wa Syria wakisherehekea ukombozi wa Halab (Aleppo) wakiwa wamebeba bendera ya Rais Bashar al Assad.

 

Katika siku za hivi karibuni, jeshi la Syria limefanikiwa kukomboa maeneo mengi ambayo yalitekwa na magaidi mwezi Machi mwaka huu. Kwa maneno mengine ni kuwa katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja, jeshi la Syria limefanyikiwa kukomboa maeneo mengi ya mkoa wa Hama kutoka mikononi mwa magaidi wanaoungwa mkono na madola ya kigeni hususan Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel. Miongoni mwa maeneo yaliyokombolewa na jeshi la Syria ni mji wa kiistratijia wa Soran. Kitongoji hicho kina umuhimu mkubwa kwani kiko katika barabara kuu inayoungania mikoa ya Homa na Halab na kinahesabiwa ni lango la kuingilia upande kaskasini mwa mkoa wa Hama. Magaidi wamepata pigo kubwa huko Syria baada ya kushindwa njama zao za kutaka kuuteka uwanja wa ndege wa kijeshi wa Hama. Katika njama yao hiyo iliyopelekea magaidi kuteka baadhi ya maeneo na kufikia hadi umbali wa kilomita 5 kutoka mji wa Hama, magaidi hao wakufurishaji walipata msaada na uungaji mkono kamili kutoka kwa nchi za Qatar, Uturuki na Saudi Arabia. Hata hivyo magenge ya kigaidi yamefurushwa kutoka kwenye maeneo yote hayo. 

Ushindi mkubwa ambao jeshi la Syria linaendelea kuupata kwa kushirikiana na waitifaki wake unathibitisha kwamba, ijapokuwa baadhi ya wakati njama za kupunguza nguvu za jeshi hilo zinawapa fursa magaidi wakufurishaji kufanya jinai zao, lakini kamwe hawafikii malengo waliyopangiwa na mabwana zao, hususan Marekani.

Tags

Maoni