• Hizbullah: Israel itashindwa vibaya zaidi katika vita vipya

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imesema kuwa, uwezo wake wa kijeshi ni jambo ambalo limeuzuia utawala haramu wa Israel kuanzisha hujuma na mashambulizi mapya dhidi ya nchi hiyo.

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah Sheikh Naim Qassim amesema, iwapo Israel itathubutu kuanzisha vita dhidi ya Lebanon basi vita hivyo kwa yakini vitamalizika kwa utawla huo wa Kizayuni kushindwa vibaya.

Sheikh Qassim amesema, chokochoko zozote za kijeshi za Israel hazitafikia malengo yoyote chanya kwa utawala huo iwe ni katika medani ya kivita au ya kisiasa.

Aprili 2 Waziri Mkuu wa Lebanon Sa'ad Hariri alionya kwamba, kuna dalili kuwa Israel ina nia ya kuanzisha vita baada ya kuzindua mfumo mpya wa makombora. Kwa upande wake Rais Michel Aoun ameutahadahrisha utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa utapata jibu kali ukitubutu kuchukua hatua yoyote ya kutoheshimu mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Wapiganaji wa Hizbullah

Itakumbukwa kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ulianzisha vita mara mbili dhidi ya Lebanon, mwaka 2000 na 2006 ambapo katika vipindi hivyo viwili, wapiganaji shupavu wa Hizbullah walitoa pigo kubwa kwa jeshi la utawala huo ghasibu ambao ulishindwa kufikia malengo yake katika vita hivyo.

Katika vita vya siku 33 vya mwaka 2006, utawala wa Kizayuni ulifanya jinai kubwa dhidi ya Lebanon ambapo uliua Walebanon 1,200 wengi wao wakiwa ni raia wa kawaida.

Apr 21, 2017 07:36 UTC
Maoni