• Saudia yaichochea FIFA iipokonye Qatar uwenyeji wa Kombe la Dunia 2022

Saudi Arabia inaziongoza nchi kadhaa za Kiarabu katika kulishinikiza Shirikisho la Soka Duniani kuipokonya Qatar haki ya kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2022 kwa madai kuwa nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi inaunga mkono ugaidi.

Taarifa katika tovutu ya Uswisi, The Local, zinasema Saudi Arabia, Yemen, Mauritania, Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri zimeandika barua zikiitaka FIFA kuipokonya Qatar haki ya kuandaa Kombe la Dunia kwa kutegema Kipengee 85 cha Sheria za FIFA ambacho kinaruhusu hatua kama hiyo ichukuliwe wakati wa dharura.

Hata hivyo mkuu wa FIFA Gianni Infantino anasema hajapokea barua hiyo hadi sasa na hivyo hawezi kutoa maoni kuhusu jambo hilo. Msemaji wa FIFA amesema shirikisho hilo la soka duniani linaendelea na mawasiliano ya kawaida na kamati ya Qatar inayoandaa Kombe la Dunia  2022.

Duru mjini Doha zinadokeza kuwa serikali ya Qatar inafahamu kuwa Saudi Arabia inaendeleza uchochezi na uhasama kuona nchi hiyo inapokonywa haki ya kuandaa kombe la dunia.

Mgogoro wa Qatar na Saudia

Ikumbukwe kuwa Jumatatu ya tarehe 5 Juni, nchi za Saudi Arabia, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu yaani Imarati na Bahrain zilitoa taarifa tofuati na kutangaza kukata uhusiano wao wa kila upande ukiwemo wa kidiplomasia na Qatar. Tarehe 23 Juni nchi hizo ziliipa masharti 13 Doha ya kurejesha uhusiano wa kawaida na nchi hizo na kuiwekea muda maalumu Qatar wa kuhakikisha imetangaza kukubaliana na masharti hayo bila ya kuhoji chochote.

Hata hivyo Qatar imeyachukulia masharti hayo kuwa yanalenga moja kwa moja kwenye uhuru wa kujitawala nchi hiyo. Wataalamu mbalimbali nao wamesema kuwa masharti hayo hayatekelezeki na inaonekana yalitolewa kwa makusudi ili kuifanya Doha ishindwe kuyatekeleza na hivyo nchi hizo nne za Kiarabu zipate kisingizio cha kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya Qatar. Kama ilivyotarajiwa, hatimaye serikali ya Doha iliwasilisha rasmi msimamo wake wa kukataa masharti hayo.

 

 

Jul 16, 2017 07:01 UTC
Maoni