• Msikiti wa al-Aqsa, lengo la njama za Israel na uhaini wa utawala wa Aal-Saud

Katika hali ambayo njama za utawala haramu wa Israel dhidi ya Masjidul-Aqsa zimeshika kasi katika siku za hivi karibuni, habari zinaripoti kuwepo harakati za utawala wa Aal-Saud kwa ajili ya kuiandalia mazingira Israel iweze kuudhibiti kikamilifu msikiti huo.

Miongoni mwa njama zinazofanywa na watawala wa Saudi Arabia dhidi ya msikiti huo ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu duniani, ni kuwashawishi na kuwashinikiza Wapalestina waachane na aina yoyote ya muqawama na mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Katika uwanja huo Ahmed Bin Saeed al-Qarni, mmoja wa mamufti wakubwa wa Saudia hivi karibuni amenukuliwa akiwataka Wapalestina na Waislamu wa dunia wawaachie msikiti wa al-Aqsa Mayahudi. Mufti huyo wa Saudia amesema wazi katika hotuba yake kwamba, nchi za Kiarabu kamwe hazitotuma jeshi lao kwa ajili ya kuukomboa msikiti huo.

Askari wa utawala haramu wa Israel wakivamia msikiti wa al-Aqsa

Matamshi hayo ya viongozi wa kidini wa Saudia kuwavunja moyo Wapalestina na hata Waislamu wengine wa dunia kuuhusu msikiti huo mtukufu, yanatolewa katika hali ambayo, kitendo cha utawala haramu wa Israel cha kuwafungia milango ya msikiti huo waumini wa Kiislamu, kimelaaniwa vikali katika fikra za waliowengi duniani hususan katika ulimwengu wa Kiislamu. Kwa kufunga milango ya msikiti huo, utawala wa Kizayuni unakusudia kutekeleza uharibifu katika eneo hilo la Kiislamu sambamba na kujenga majengo na maeneo ya Kiyahudi ndani ya msikiti huo na hivyo kubadili kabisa muundo wa Kiislamu wa msikiti huo kuwa na sura ya Kiyahudi. Kuhusiana na suala hilo, Khalil al-Tafkaji mtaalamu wa masuala ya Palestina eneo la Quds amesema kuwa, viongozi wa utawala wa Kizayuni wanafanya njama ya kufikia malengo yao ya kistratijia na ya muda mrefu ya kuunda utawala wao wa kilowezi katika mji wa Quds.

Askari wa Kizayuni wakiwazingira Waislamu wanaoswali msikitini hapo

Ameongeza kuwa, kitendo cha Israel cha kufunga milango ya msikiti wa al-Aqsa ni katika kutekeleza malengo ya kisiasa na kwamba, moja ya malengo hayo ni kujenga kanisa la Kiyahudi katika eneo la Bab al-Rahma ndani ya uwanja wa msikiti huo. Akizungumzia kuhusika mataifa ya Kiarabu na njama hiyo ya kufungwa milango ya msikiti huo Khalil al-Tafkaji amesema: "Utawala wa Kizayuni unatumia vibaya tofauti zilizopo baina ya nchi za Kiarabu kwa ajili ya kufikia malengo yake. Hii ni kwa kuwa viongozi wa mataifa hayo ya Kiarabu wanasisitizia kuendelezwa mahusiano yao ya wazi na yasiyo ya wazi na utawala wa Kizayuni kwa kudhani kwamba kufanya hivyo kutawasaidia kuendelea kusalia madarakani. Lakini wanasahau kuwa, wakati muundo wa Quds utakapokamilika na kuwa wa Kiyahudi, watawala wote wa Kiarabu kuanzia mashariki hadi magharibi, watang'olewa madarakani na utawala huo huo wa Kizayuni." Mwisho wa kunukuu.

Mfalme Salman wa Saudia akicheza densi na Trump kufurahia njama zao

Naye kwa upande wake Ahmad al-Nifar, msomi mtajika wa Kiislamu wa nchini Tunisia amesema: "Hivi sasa Waislamu tunakabiliwa na tukio hatari sana katika msikiti wa al-Aqsa. Wazayuni kwa kutumia vibaya matukio yaliyojitokeza katika nchi za Kiarabu, wanataka kuudhibiti kikamilifu msikiti wa al-Aqsa kutokana na nafasi muhimu ulionayo kiutamaduni, kihistoria na kimaanawi kati ya Waislamu duniani." Ameongeza kwa kusema: "Kwa bahati mbaya, hatua hatari za utawala vamizi wa Kizayuni katika msikiti wa al-Aqsa zinafanyika katika hali ambayo nchi za Kiarabu zimeungana na utawala huo huo wa Kizayuni dhidi ya matakwa ya Waarabu wenzao." Mwisho wa kunukuu. Hatua ya utawala wa Aal-Saud ya kupuuza haki ya raia madhlumu wa Palestina na kadhalika upuuzaji wake wa suala zima la Quds ambacho ni kibla cha kwanza cha Waislamu duniani, inatekelezwa katika hali ambayo utawala huo wa Saudia unajidai kuwa eti wenyewe unatumikia Uislamu. Hii ni katika hali ambayo Saudia kwa kuwasilisha mpango eti wa amani wa Kiarabu, inatekeleza kwa makusudi njama chafu za Wamagharibi na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na kuimarisha zaidi nafasi ya Israel huko Palestina na eneo  zima la Quds.

Askari wa Kizayuni wakiwashambulia waumini msikitini hapo

Ni kutokana na hilo huo ndio maana watawala wa Aal-Saud wakaamua kukaa kimya na kutochukua hatua yoyote ya kulaani hujuma za utawala wa Kizayuni hususan katika eneo la Quds. Bali kinyume chake Saudia inashirikiana wazi wazi na Israel ambapo hata katika maandamano ya wananchi wa Saudia katika Siku ya Kimataifa ya Quds, askari wa utawala wa Aal-Saud waliwamiminia risasi waandamanaji hao ambao walikuwa wakiandamana kwa amani kuutetea msikiti huo na hivyo Riyadh ikawa imewathibitishia walimwengu kwamba, inatekeleza siasa za Tel Aviv. Watawala wa Saudia ambao wanajiarifisha duniani kama viongozi wa Kiislamu, badala ya kuutumikia umma wa Kiislamu,  wameikabidhi nchi hiyo kwa maadui wa Uislamu, yaani utawala wa Kizayuni, mienendo ambayo haina maana nyingine ghairi ya kuufanyia hiyana umma wa Kiislamu. Hata hivyo kuendelea muqawama na mapambano ya Wapalestina zikiwemo operesheni za kujitolea kuuawa shahidi, yamethibitisha kwamba, Uzayuni na Uwahabi licha ya juhudi na njama kubwa zinazofanyika lakini hauwezi kuwatenga Wapalestina na Waislamu kwa ujumla kunako matukufu yao na masuala ya ulimwengu wa Kiislamu, hususan kadhia ya Quds.

Jul 16, 2017 12:19 UTC
Maoni