• Sisitizo la Rais Erdoğan wa Uturuki la kuendeleza siasa za kukabiliana na wapinzani wa serikali

Katika kutimia mwaka mmoja tokea jaribio la mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli nchini Uturuki, Rais Recep Tayyip Erdoğan wa nchi hiyo amesema serikali yake itaendelea kutekeleza siasa za kupambana na wapinzani wa serikali yake.

Rais Erdoğan ameyasema hayo katika kumbukumbu za mwaka mmoja tangu kujiri mapinduzi ya kijeshi ambayo hata hivyo yalifeli hapo tarehe 15 Julai mwaka jana ambapo pamoja na mambo mengine amesisitizia udharura wa kile alichokitaja kuwa ni kupandishwa mahakamani na kuchukuliwa hatua kali wale wote waliohusika kwa namna moja au nyingine na mapinduzi hayo. Aidha amesema kwa mara nyingine Ankara haitoruhusu kundi lolote kama lile la Fethullah Gülen kuendesha harakati zake nchini humo. Licha ya Rais Recep Erdoğan na viongozi wengine wa ngazi za juu wa Uturuki kulihusisha kundi la Fethullah Gülen na mapinduzi hayo ya kijeshi, lakini viongozi wa kundi hilo akiwemo Gülen mwenyewe wamekanusha tuhuma hizo za serikali ya Ankara.

Vurugu zilizojiri siku ya jaribio la mapinduzi ya Julai 15 2016

Hakuna shaka kwamba serikali ya Uturuki inatekeleza ukandamizaji mkubwa dhidi ya wapinzani wake kupitia propaganda za mapinduzi hayo. Sambamba na kumbukumbu za mapinduzi hayo, Wizara ya Vyombo Vya Sheria ya Uturuki imetangaza kuwa, watu ambao wamefuatiliwa kwa kuhusika kwa namna yoyote na mapinduzi hayo wanakaribia laki moja na elfu 70. Kwa mujibu wa wizara hiyo, majenerali wa jeshi 169 na askari 7098 ambao akthari yao wana vyeo vya kanali, wanaendelea kushikiliwa katika korokoro za nchi hiyo. Aidha ripoti hiyo imesema kuwa, jumla ya magavana wa zamani 24 na manaibu wao wapatao 73, wakuu wa mikoa 116 na wafanyakazi 8815 wa idara tofauti za serikali, wanaendelea kushikiliwa na polisi ya Uturuki. Propaganda kubwa za serikali ya Ankara sambamba na kumbukumbu ya mwaka mmoja wa mapinduzi ya kijeshi nchini humo zimekuwa na taathira hasi nyingi.

Siku ya mapinduzi hayo Edugan alizungumza kwa simu akiwa mafichoni

Katika uwanja huo, Doğu Perinçek kiongozi wa chama cha Kitaifa kwa ajili ya Uturuki ameitaka serikali ya nchi hiyo kukomesha propaganda hizo huku akimtaka pia Rais Erdoğan ajiuzulu madarakani. Serikali ya Uturuki inadai kuwa, Fethullah Gülen kwa kutumia kundi lake ambalo limepenya katika idara tofauti za serikali kuanzia vyombo vya mahakama, jeshi, idara za masomo na asasi nyingine za serikali, alipanga na kuratibu mapinduzi hayo ya mwaka jana, katika hali ambayo kwa mara kadhaa Fethullah Gülen mwenyewe amekanusha tuhuma hizo na kuzitaja kuwa zisizokuwa na ukweli wowote. Hii ni katika hali ambayo wajuzi wa mambo na hata vyombo mbalimbali vya kieneo na kimataifa vimebaini kwamba serikali ya Imarati ilihusika katika mapinduzi hayo yaliyofeli nchini Uturuki.

Rais Recep Tayyip Erdoğan

Aidha duru hizo zimefichua namna ambavyo Imarati ilifadhili kifedha mapinduzi hayo na kwamba pamoja na hayo lakini bado Uturuki haitaki kuihusisha serikali ya Abu Dhabi na tukio hilo. Itakumbukwa kuwa mwaka jana David Hartz, mwandishi mashuhuri wa habari na muhariri wa zamani wa gazeti la The Guardian, sambamba na kufichua ripoti kuhusiana na suala hilo aliandika kuwa, Imarati iliunga mkono kifedha mapinduzi ya tarehe 15 Julai 2016 nchini Uturuki. Kwa upande wake Omar Dogli mwandishi wa habari wa gazeti la Yeni Shafag la nchini Uturuki ameandika makala inayosema: "Serikali ya Imarati ilitoa kiasi cha Dola bilioni tatu kwa ajili ya kuing'oa madarakani serikali ya Rais Erdoğan kwa kuwanunua baadhi ya watu wa Fethullah Gülen." Mwisho wa kunukuu. Matamshi ya Rais Erdoğan dhidi ya Gülen yanatolewa katika hali ambayo chama tawala cha Uadilifu na Ustawi cha Uturuki ndicho kinachohusika pakubwa katika kupanuka na kuenea kwa kundi la Fethullah Gülen katika ulimwengu wa Kiislamu na hata katika nchi ambazo zina mahusiano mazuri na Uturuki. Hata hivyo miaka michache iliyopita, Uturuki imekuwa ikiendesha vita vya kuwania madaraka kati ya chama tawala na kundi la Fethullah Gülen.

Doğu Perinçek kiongozi wa chama cha upinzani anayemtaka Erdogan ajiuzulu

Katika uwanja huo tangu kilipoingia madarakani hapo mwaka 2003, chama tawala kimekuwa kikilitangaza kundi la Fethullah Gülen katika nchi tofauti za dunia kuwa lisilofaa. Hii ni katika hali ambayo akthari ya viongozi wa serikali na hata wapambe wa Rais Erdoğan mwenyewe walisoma katika shule zinazomilikiwa na Gülen. Kiujumla tunaweza kusema kuwa, matamshi ya hivi karibunia ya Rais Tayyip Erdoğan yanaweza kutajwa kuwa ni namna fulani ya kuwatisha raia wa Uturuki kunako kundi la shakhsia huyo, kama ambavyo pia yanaonekana kuwa ni njia ya kuwakandamiza wapinzani wa serikali na chama tawala.

 

 

Jul 17, 2017 04:21 UTC
Maoni