• Marekani: Waimarati ndio waliozusha balaa kwa kudukua mitandao ya Qatar

Maafisa wa kijasusi wa Marekani wamesema kuwa, uchunguzi wao wa kiitelijensia umegundua kuwa, Umoja wa Falme za Kiarabu yaani Imarati ndio uliodukua mitandao ya Intaneti ya serikali ya Qatar na kuingiza maneno ya uongo ili yaonekane yamesemwa na Amir wa Qatar, Tamim bin Hamad Aal Thani.

Gazeti la Washington Post la nchini Marekani limemnukuu afisa mmoja wa kijasusi wa nchi hiyo akifichua kuwa, Umoja wa Falme za Kiarabu ulidukua mitandao ya intaneti ya serikali ya Qatar kwa lengo la kueneza habari za uongo na kuzinasibisha na Amir wa nchi hiiyo Sheikh Tamim bin Hamad Aal Thani, suala ambalo ndilo lililowasha moto wa kuwekewa vikwazo vya kila upande Qatar na nchi nne za Kiarabu za Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri.

Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Aal Thani (kushoto) akikaribishwa mjini Riyadh na mfalme wa Saudia, Salman bin Abdulaziz Aal Saud. Ugomvi wa muda mrefu wa pande hizo mbili uliripuka baada ya rais wa Marekani Donald Trump kutembelea Riyadh mwezi Mei 2017

 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wiki iliyopita, maafisa wa Marekani walipata taarifa mpya za kijasusi zilizokusanywa na mashirika ya kijasusi ya nchi hiyo ambazo zinathibitisha kwamba tarehe 23 Mei mwaka huu, viongozi wa ngazi za juu wa serikali ya Imarati walizungumzia mpango huo.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa, haijulikani iwapo viongozi wa Imarati ni wao wenyewe waliotekeleza mpango huo au waliwatumia watu wengine. Kama ambayo haijulikani pia iwapo nchi nyingine za Kiarabu kama vile Saudi Arabia zilishiriki kwenye operesheni hiyo au la.

Maelezo yaliyojitokeza kwenye kurasa za Intaneti za mitandao ya serikali ya Qatar yalidai kuwa, Amir wa nchi hiyo amesema, Iran ni dola lenye nguvu la Kiislamu na kuisifu pia Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS. Doha ilikanusha habari hiyo na kusema mitandao yake imedukuliwa. Hata hivyo nchi za Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri zilikataa ukanushaji huo wa Doha na zilichukua hatua kali za kukata uhusiano wa kila upande, wa angani, baharini, ardhini, kidiplomasia, kibiashara na kila kitu kati yao na Qatar.

Bendera za nchi za Saudia na Bahrain (juu), Imarati na Misri (chini) zikiwa zimeizingira katikati bendera ya Qatar

 

Gazeti la Washington Post la nchini Marekani limeongeza kuwa, mitandao ya serikali ya Qatar ilidukuliwa tarehe24 Mei mwaka huu, siku chache tu baada ya rais wa Marekani Donald Trump kutembelea Saudi Arabia na kuonana na viongozi wa nchi kadhaa za Kiarabu.

Kwa upande wake, Yousef al-Otaiba, balozi wa Imarati nchini Marekani amedai kuwa taarifa hiyo iliyochapishwa na gazeti la Washington Post ni uongo. Amesema, Abu Dhabi haijahusika kivyovyote vile na udukuzi unaodaiwa kufanywa katika mtandao ya Intaneti ya serikali ya Doha.

Amedai kuwa, tuhuma zinazoikali Qatar ni kuunga mkono ugaidi na misimamo mikali na kudhoofisha utulivu wa majirani zake. 

Jul 17, 2017 07:10 UTC
Maoni