• Kuzidi kutokota mgogoro ndani ya Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi

Baada ya Rex Tillerson, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kushindwa kupatanisha mgogoro wa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi ulioanzishwa na Saudi Arabia dhidi ya Qatar, maafisa wa kijasusi wa Marekani wametangaza kuwa, Umoja wa Falme za Kiarabu yaani Imarati ndiyo iliyodukua mitandao ya Intaneti ya Qatar na kuzua mgogoro uliopo hivi sasa.

Maafisa hao wa kijasusi wa Marekani wamesema kuwa, uchunguzi wao wa kiitelijensia umegundua kwamba, Umoja wa Falme za Kiarabu yaani Imarati ndio uliodukua mitandao ya Intaneti ya serikali ya Qatar na kuingiza maneno ya uongo ili yaonekane yamesemwa na Amir wa nchi hiyo, Tamim bin Hamad Aal Thani. Gazeti la Washington Post la nchini Marekani limemnukuu afisa mmoja wa kijasusi wa nchi hiyo akifichua kuwa, Umoja wa Falme za Kiarabu ulidukua mitandao ya Intaneti ya serikali ya Qatar kwa lengo la kueneza habari za uongo na kuzinasibisha na Amir wa nchi hiiyo Sheikh Tamim bin Hamad Aal Thani, suala ambalo ndilo lililowasha moto wa kuwekewa vikwazo vya kila upande Qatar na nchi nne za Kiarabu za Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri.

Usalama wa Taifa: Imarati ilidukua mitandao ya serikali ya Qatar na kuzusha mabadiliko ya kutisha kieneo, kwa mujibu wa maafisa wa kijasusi wa Marekani

 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wiki iliyopita, maafisa wa Marekani walipata taarifa mpya za kijasusi zilizokusanywa na mashirika ya kijasusi ya nchi hiyo ambazo zinathibitisha kwamba tarehe 23 Mei mwaka huu, viongozi wa ngazi za juu wa serikali ya Imarati walizungumzia mpango huo. Gazeti la Washington Post la nchini Marekani limeongeza kuwa, mitandao ya serikali ya Qatar ilidukuliwa tarehe 24 Mei mwaka huu, siku chache tu baada ya rais wa Marekani Donald Trump kutembelea Saudi Arabia na kuonana na viongozi wa nchi kadhaa za Kiarabu. Maelezo yaliyojitokeza kwenye kurasa za Intaneti za mitandao ya serikali ya Qatar yalidai kuwa, Amir wa nchi hiyo amesema, Iran ni dola la Kiislamu lenye nguvu na pia aliisifu Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS. Doha ilikanusha habari hiyo na kusema mitandao yake imedukuliwa. Hata hivyo nchi za Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri zilikataa ukanushaji huo wa Doha na zilichukua hatua kali za kukata uhusiano wa kila upande, wa angani, baharini, ardhini, kidiplomasia, kibiashara na kila kitu kati yao na Qatar. Kwa mtazamo wa maafisa wa kijasusi wa Marekani, kwa uchache nchi za Saudia, Imarati na Misri ndizo zilizohusika kwenye udukuzi huo. 

Amma jambo ambalo halina shaka hata kidogo ni kwamba hakuna tena kuaminiana wanachama sita wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi. Mashambulizi makali ya maneno yaliyopo hivi sasa baina ya viongozi wa nchi hizo yanathibitisha ukubwa wa mgogoro uliokita ndani ya baraza hilo. Weledi wa mambo wanasema kuwa, vurugu zote hizi zinatokana na siasa mbovu za watawala wa ukoo wa Aal Saud ambao wamezoea kuendesha siasa za kidikteta hata nje ya Saudia. Kosa kubwa lililofanywa na Saudia ni kumwalika mjini Riyadh mtu kama Donald Trump ambaye hafichi uadui wake kwa Waislamu. Viongozi wa Aal Saud walidhani kuwa wataweza kuagua ndoto yao ya kuanzisha muungano wa kuipiga vita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa uungaji mkono wa Donald Trump. Hata hivyo, hata baada ya Donald Trump kukubali ndege yake itue kwanza mjini Riyadh kabla ya kuelekea kokote katika safari yake ya kwanza nje ya Marekani tangu atangazwe kuwa rais wa nchi hiyo, lakini aliyenufaika ni Trump tu kwa hongo ya mabilioni ya dola aliyopewa na Saudia kwa visingizio tofauti kama vile zawadi na mikataba ya kijeshi. Matunda pekee ya ziara hiyo ya Trump nchini Saudi Arabia ni mgogoro mkubwa uliozuka ndani ya Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi.

Rais wa Marekani, Donald Trump akicheza ngoma ya upanga na mfalme wa Saudia, Salman bin Abdulaziz Aal Saud. Inasemwa kuwa,  ngoma hiyo ilichezwa chini ya kivuli cha kuchezea uhuru wa nchi kama Qatar, Kuwait na Oman

 

Hii ni kusema kuwa ngoma ya upanga ya mfalme wa Saudia na Donald Trump ilichezwa chini ya kivuli cha kuchezea uhuru wa nchi kama Qatar, Kuwait na Oman. Wachambuzi wa mambo wanasema, Marekani ndiyo inayochochoe mizozo kati ya nchi za Ghuba ya Uajemi ukiwemo mgogoro wa hivi sasa ulioanzishwa na Saudi Arabia dhidi ya Qatar. Gazeti la al Quds al Arabi linalochapishwa mjini London Uingereza limeandika: Muungano ulioanzishwa na Saudia dhidi ya Qatar umewaparaganya wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na kuna uwezekano wa kuundwa muungano mwingine mpya katika eneo hili.

Amma jambo ambalo viongozi wa Saudi Arabia hawapendi kulisikia ni kwamba, ushirikiano na kuwa na fikra moja nchi za eneo fulani, hakuna maana ya kuzipoka nchi hizo uhuru wao wa kuamua zinachopenda. Siasa za kuheshimiana na kuachiwa kila nchi kuchukua maamuzi kwa uhuru kamili ndizo zinazoweza kudhamini usalama na utulivu wa eneo hili. Ikumbukwe kuwa kila nchi inaingia katika milingano ya kisiasa kwa kuzingatia kwanza uhuru na heshima yake na hivi sasa zimeisha tena zile zama za kuzifanyia udikteta wa kisiasa nchi nyinginezo.

Jul 17, 2017 09:58 UTC
Maoni